Mwenyekiti wa muda wa Chama Cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro
amesema kuwa hatawania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika
uchaguzi unaopangwa kufanyika hivi karibuni.
Mtatiro alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa muda wa chama hicho akikalia
nafasi iliyoachwa na Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu mwaka jana na
baadae mwaka huu kuzua sintofahamu baada ya kutengua uamuzi wake na
kutaka kurejeshewa nafasi hiyo.
“Sina mpango wa kuwania nafasi ya uenyekiti wa CUF hivi karibuni,”
Mtatiro anakaririwa na Mwananchi. “Nitaendelea kuitumikia CUF kama
mwanachama mtiifu,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa muda alisema kuwa anaunga
mkono mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuitisha
maandamano nchi nzima Oktoba 1 mwaka huu baada ya kuahirisha kufanya
hivyo Septemba 1 kupitia kile wanachokiita Oparesheni UKUTA.
“Ninawapongeza Chadema kwa kusogeza mbele maandamano hadi Oktoba 1 ili kupata muda zaidi wa ushauri,” alisema.
“Kwa niaba ya wanachama wa CUF na watu wanaotuunga mkono ninatangaza
kuwa tutashiriki katika maandamano hayo,” Mtatiro anakaririwa.
Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku kufanyika kwa maandamano na
mikutano ya kisiasa nchi nzima na tayari imewashikilia, kuwahoji na
kuwafungulia mashtaka baadhi ya viongozi wa Chadema waliohusika kuandaa
maandamano hayo.
Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa na mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa chama hicho
pia walihojiwa na Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment