Kamishna wa Polisi
Kanda Maalum Dar Es Salaam anatoa rai kwa wakazi wa Jiji la Dar Es salaam na
wageni wanaoingia jijini wakitokea mikoani
kupuuza taarifa za sauti zinazozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa
Polisi wanawakamata ovyo watu wanaolala kwenye nyumba za kulala wageni.
Taarifa hizo za
uvumi zinazoendelea kuzagaa kwenye mitandao ya Kijamii kama WHATSAPP, TELEGRAM na pia zimechapishwa
kwenye baadhi ya magazeti kwamba Askari Polisi wanawakamata watu ovyo mchana wakiwa kwenye nyumba za kulala
wageni kwa madai ya kukamata kwa makosa
ya uzembe na uzururaji na pia kutimiza kauli ya Raisi wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania ‘HAPA NI KAZI TU’.
Kimsingi
niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na oparesheni za kuwasaka watuhumiwa wa
makosa mbalimbali yakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni
kinyume cha sheria (guest bubu), mjambazi
na wahalifu wengine wa makosa mbalimbali.
Aidha taarifa za kuaminika zimebaini kuwa baadhi
ya nyumba za kulala wageni zimekuwa zikitumika kuhifadhi magenge ya wahalifu,
dada poa na kaka poa, hivyo Jeshi la Polisi tunawajibika kufuatilia na
kuwakamata wahalifu.
Niwajibu wa
Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za kulala wageni, Hoteli,
migahawa, Vilabu vya vileo, kumbi za
starehe zinazokesha na zisizokesha na watakaobainika kuvunja sheria, hatua kali
za kisheria dhidi yao zitachukuliwa. Sheria ya Mwenendo ya makosa ya jinai kifungu
cha 60(1) (sura ya 77 iliyofanyiwa
marekebisho 2002) kinampa nguvu askari kufanya ukaguzi wa maeneo yote
yaliyotajwa hapo juu na kumkamata mtu yeyote anayetiliwa shaka akienda kinyume
na utaratibu wa biashara hizo.
Sambamba na
hayo nawatahadharisha wafanyabiashara wote wa nyumba za kulala wageni wafuate
taratibu za kupokea wageni kwa kuandika kwenye vitabu, kuandika namba za
vitambulisho vyao na sehemu wanayotoka, na pale watakapomtilia mashaka mteja yeyete
watoe taarifa kituo chochote cha polisi.
Pia wenyeviti
wa serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi wanawajibika kuwatambua wageni
wote wanaoingia kwenye himaya zao na kuwachukulia hatua stahiki ili kuimarisha
usalama katika jiji letu la Dar Es
salaam.
DAR
ES SALAAM BILA UHALIFU INAWEZEKANA, TUSHIRIKIANE KUISAFISHA JIJI LETU
S.N.SIRRO - CP
KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment