Wednesday, September 7, 2016

KUTOKA BUNGENI--Watumishi wameaswa kuwasilisha nyaraka zao mapema kabla ya muda wa kustaafu.

index
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO, Dodoma.
Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti 2016 imefanikiwa kulipa jumla ya sh. bilioni 511.86 ikiwa ni malimbikizo ya mwajiri kwa watumishi waliostaafu.


Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mary Chatanda Mbunge wa Korogwe Mjini aliyehoji kuhusu changamoto
    Mary Chatanda Mbunge wa Korogwe mjini
inayowakabili wastaafu ya kucheleweshewa mafao yao na Mfuko wa pensheni wa PSPF katika mwaka wa fedha 2015/2016.

“Kucheleweshwa kwa malipo ya wastaafuhakutokani na Serikali, isipokuwa waajiri ndio baadhi ya nyaraka zinazohusika ili kuaandaa malipo ya wastaafu hao alisema Dkt. Kijaji.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji amesema kuwa nyaraka zinazomhusu mtumishi ziwasilishwe ndani ya muda wa miezi mitatu hadi sita kabla ya muda wa kustaafu ili malipo yake yaweze kuandaliwa kwa wakati na kupata stahili zao ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Aidha, jumla ya sh. bilioni 83.25 zimelipwa ikiwa ni malipo ya deni kabla ya mwaka 1999 hali inayoonesha kuwa Serikali inaendelea kulipa malimbikizo ya madai ya wastaafu na mafao mengine yanayotolewa na Mfuko huo ili waweze kuendesha maisha yao baada ya kustaafu.

Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai 2016 Mfuko umelipa mafao ya pensheni ya mwezi kwa kiasi cha sh. bilioni 117 ambapo kwa sasa mfuko huo unaendelea kulipa malimbikizo ya mafao ya mkupuo kwa wastaafu wapya na mafao mengine.

Katika kudhihirisha dhamira hiyo ya kulipa mafao ya wastaafu, Dkt. Kijaji amesema kuwa tangu Julai 2015 bodi za mifuko ya hifadhi za jamii zinaendelea kufanyia kazi mafao ya wastaafu na kuwalipa stahili zao kwa asilimia 50 kulingana na maelekezo ya Serikali.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Muhagama ameliarifu Bunge kuwa mfumo na sheria vimeunganishwa na kutoa fursa kwa mtumishi anapohama kutoka ajira moja kwenda nyingine anaruhusiwa kuhama kutoka mfuko moja kwenda mfuko mwingine.

No comments: