MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Deogratius Ndejembi
amekifunga Chuo cha Ualimu cha Nkuruma kilichopo Mkoka na kuagiza
uongozi wa chuo kurudisha fedha zote za ada walizolipa wanafunzi ili
ziwasaidie kulipia vyuo vingine.
Alitoa agizo hilo wakati wa mkutano na wanafunzi pamoja na uongozi wa
chuo hicho kuhusu kutafuta suluhu ya mgogoro ambao ulianza Septemba 16,
mwaka huu. Chuo hicho kilidahili wanafunzi 77 kwa lengo la kuwafundisha
ualimu, walipofika wakaambiwa wanasoma masomo ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (ICT).
“Baadaye wakaambiwa wanabadilishiwa masomo sasa wanasoma Maendeleo ya
Jamii, hii yote wamefanya kwa kuwa chuo hakina usajili wowote.Ada
wamechukua na hakuna kinachoendelea,” alisema Ndejembi.
Ndejembi alifikia hatua ya kukifunga chuo kutokana na wanafunzi
kugoma kufanya mitihani ya chuo ya kumaliza mwaka wa masomo kwa madai
chuo hakitambuliwi na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Alisema kukifungia chuo pekee haitoshi wanatakiwa kurudisha fedha
zote za ada walizolipwa na wanafunzi katika mwaka huo wa masomo uliopita
ili kuwasaidia kulipa vyuo vingine.
“Kuwarudishia fedha sio mwisho wa jambo hili kwa sababu mmepotezewa
muda wenu na haki yenu ,mmeonewa, mmedhulumiwa kwa kusema hivyo
namwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya na timu yake kuwakamata sasa hivi na
wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria ili haki iweze kutendeka,”
alisema.
Amewataja wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni mmiliki
wa chuo, Mathew Nkurlu, Msajili wa Chuo, Yohana Michael, Mhasibu Elieth
Ruben, wakufunzi Pendael Petro na Christopher Mabatian.
Ndejembi alitaja sababu za kuagiza wakamatwe viongozi hao wa chuo ni
kuwa walihusika kushiriki katika kufanya udanganyifu na kuwatapeli
wanafunzi hao huku wakijua kinachoendelea.
Aidha, alisema serikali itawasaidia katika utaratibu wa kupata vyuo
vingine kwa wale wenye sifa za kujiunga na vyuo katika kozi ambayo
walianza kusoma.
Alisema kama ikitokea chuo hakina fedha za kuwarudishia wanafunzi,
majengo yao yatatumika kama dhamana ya ada kwa vyuo ambavyo vitawapokea
wanafunzi hao. Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Mhoja
Matando aliishukuru serikali kwa kuwasaidia kujua hatma ya kutimiza
ndoto yao ya kielimu.
No comments:
Post a Comment