SERIKALI:KUELEKEA MABADILIKO YA UENDESHWAJI WA VILABU VYA SIMBA NA YANGA MICHAKATO ILIYOKUWA IKENDELEA MARUFUKU
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja.
……………………………………………………………
Na.Alex Mathias,Dar es salaam.
Baraza la Michezo la Taifa limeagiza
michakato yote inayoendelea kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa
Wanachama kwenda kwenye umiliki wa hisa na ukodishwaji kwa vilabu vyote
vya michezo usitishwe mara moja hadi marekebisho ya katiba zao kwa
mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na kanuni za Msajili
Namba 442 kanuni ya 11 ya kifungo kidogo cha 1-9 yatakapofanyika.
Akizungumza na waandishi wa Habari
Katibu Mkuu wa BMT Mohamed Kiganja, amesema kuwa baraza linapenda kuona
kwamba wahusika wakuu wa jambo hilo hasa klabu za Simba na Yanga
wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao.
Aidha amesema kuwa endapo vilabu hivyo
kama vitaendelea na mchakato huo kabla ya taratibu za kurekebisha katiba
zao kisheria ni kosa na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya
watakaokiuka maelezo hayo.
“Hivi karibuni imeibuka michakato ya
watu wakitaka kubadilisha umiliki wa vilabu vya wanachama na kuvielekeza
kwenye utaratibu wa hisa na ukodishwaji,vitendo hivi vimesababisha
migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani ndani ya tasnia ya
michezo kwani imefikia hatua watu wanaenda mahakamani mfano mzuri ndani
ya klabu ya Yanga”alisema Kiganja.
Ameongeza kuwa makundi ya wapenzi na
wanachama wamejikita katika mijadala ambayo hatma yake ni kuzidi
kuibomoa jamii badala ya kuijenga na kuimalisha michezo nchini.
Aidha amesema kuwa kuna mipasuko ambao
umepelekea baadhi ya wanachama wameona kuwa hawaridhishwi na mwenendo
mzima na pengine hata taratibu za suluhu zilikiukwa na kuona hazifai na
kuamua kukimbilia Mahakamani.
“Kutokana na hali hiyo BMT kama chombo
pekee cha kisheria kilichopewa dhamana ya kusimamia Michezo
nchini,hakiwezi kuvumilia ukiukwaji wa Sheria na taratibu zinazoendelea
na kuashiria kutoweka kwa amani kwenye tasnia ya Michezo”alisema
Kiganja.Hivyo basi,Baraza linasitisha michakato yote inayoendelea ya
kutaka kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwenye mfumo ulipo sasa na ni
vyema vilabu vikaendelea kubaki kuwa mali ya Wanachama.
“Kama kuna mdau yeyote ambaye ana nia ya
kumiliki klabu ya Mchezo wowote ule ni vyema akaanzisha timu yake kama
bwana Said Salim Bhakhresa alivyoamua kuanzisha klabu ya Azam FC”alisema
Kiganja
No comments:
Post a Comment