Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu Dkt. John Magufuli amewaongoza Watanzania katika maadhimisho ya sherehe za miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania bara.
Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es saalam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Sherehe hizo zilipambwa na gwaride, ngoma za asili, wimbo maalumu kutoka vikosi vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi.
Katika hatua hiyo, kikosi maalumu cha wanamaji kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania walionesha umahiri wao kwa kupita mbele ya Rais huku wakibeba mabegi yenye uzito wa kilo 65 za vifaa vinavyowawezesha kuhimili maisha ndani ya siku saba wawapo katika uwanja wa medani bila kuhitaji msaada wowote.
Kwa upande wa Kikosi cha Komandoo wa Jeshi la Nchi Kavu walionesha uwezo wao wa kufanya vitendo tofauti wakati wa kupambana na maadui wawapo vitani.
Sherehe hizo zilijaa shamrashamra baada ya kwata ya kimya kimya kutoka kikosi cha maadhimisho cha Jeshi la Wananchi wenye uzito chini ya kilo 50 kuingia uwanjani hapo ambapo walionesha umahiri wao wa kuweza kucheza na silaha.
Baada ya kwata hizo ngoma za asili zilizobeba ujumbe wa siku ya uhuru kutoka Mbeya, Lindi, na Unguja Kaskazini zilifuatia kwa ajili ya kutumbuiza.
Kabla ya kumalizika kwa sherehe hizo, Rais Magufuli alipata fursa nafasi ya kuzungumza na Watanzania ambapo aliwaasa kuendeleza kudumisha umoja, upendo, amani na mshikamano baina yao.
Kauli mbiu ya sherehe hiyo ni “Tuunge Mkono Jitihada Za Kupinga Rushwa na Ufisadi na Tuimarishe Uchumi wa Viwanda kwa Maeneleo yetu”.
No comments:
Post a Comment