Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison
Mwakyembe amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga mahakama za
mwanzo katika kila kata nchini ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa
wananchi.
Mhe. Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo alipotembelea ujenzi wa
Mahakama ya kisasa ya Wilaya Kigamboni inayojengwa kwa kutumia teknolojia ya
Moladi ambayo inapunguza muda na gharama za ujenzi ambayo inagharimu kiasi cha
shilingi milioni 572 na ujenzi wake unatarajiwa
kukamilika ifikapo Februari 2017.
Waziri Mwakyembe amesema moja ya kipaumbele cha Wizara yake ni
kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi hivyo huduma za kimahakama
zitaendelea kuboreshwa na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile amesema anaishukuru Serikali kwa kujenga Mahakama ya kisasa Kigamboni
na hivyo kusogeza huduma kwa wananchi na pia ameipongeza Serikali kwa kuanzisha
mchakato wa kutunga Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ambayo itasaidia
sana wananchi wa kipato cha chini.
Aidha, Mhe. Ndugulile ameomba changamoto za ucheleweshwaji wa
kesi Mahakamani na rushwa ziweze kutafutiwa ufumbuzi maana ni miongoni mwa kero
zinazowakabili wananchi.
No comments:
Post a Comment