Monday, January 9, 2017

Umeiona Hii ya Rais Dkt.Magufuli leo huko chato?

chato-2Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 9 Januari, 2017 amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato,ambapo ndipo aliposoma kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kuzungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Rais Dkt Magufuli ameahidi kujenga madarasa matatu na ofisi moja ya walimu katika Shule hiyo kufuatia ombi la Walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.
Aidha Dkt.Magufuli amewaasa wanafunzi kutilia mkazo masomo ili waweze kufaulu na kuwataka walimu kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na Serikali kila mwezi katika kutoa elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa kama ilivyo kwa baadhi ya shule ambazo zimegundulika kuwa na wanafunzi hewa katika uhakiki uliofanywa na serikali.
chato-4
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Chato mkoani Geita. Shule hiyo ya Msingi Chato ndiyo Rais Dkt. Magufuli alisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka Darasa la Saba. Rais Dkt. Magufuli amewaasa Wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwasababu yeye pia alisoma shuleni hapo. Picha na Mpigapicha Maalum
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chato, Bwana Mwita Chacha amemshukuru Rais Dkt.Magufuli kwa msaada aliowapatia katika kukabiliana na uhaba wa madarasa uliokuwa unaikumba shule hiyo, pia kuitembelea Shule yao jambo ambalo limewatia moyo walimu na wanafunzi shuleni hapo.
Rais Magufuli pia ametembelea eneo la Stand ya zamani na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwepo eneo hilo na kutoa msaada kwa kikundi cha wasafisha viatu ili kuongeza mtaji wa biashara yao.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita.
9 Januari, 2017

No comments: