Baada ya Simba kutangulia robo fainali ya Kombe la Shirikisho la
Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup kwa kuifunga African Lyon kwa bao
1-0, mechi nyingine za kuwania nafasi hiyo zitaanza kuchezwa kesho Ijumaa
Februari 24, mwaka huu.
Simba iliilaza African Lyon katika mchezo wa hatua ya 16 bora
uliofanyika Februari 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Michezo ya kesho kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT
Ruvu ya Pwani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha
wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma
na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea
ilihali Azam na Mtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala, Dar es Salaam. Michezo
yote itaanza saa 10.00 jioni.
Jumapili Februari 26, mwaka huu timu ya Mbao FC itacheza na
Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania
Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini
Mbeya.
Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment