Monday, March 13, 2017

HABARI ZOTE MPYA KUTOKA TFF ZIPO HAPA LEO

MALINZI AMLILIA SIR GEORGE KAHAMA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, ametuma rambirambi kwa familia ya marehemu Sir George Kahama aliyefariki dunia Jumapili akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Rais Malinzi amesema taifa limepoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania maendeleo ya mpira wa miguu baada ya kupigania Uhuru ambao Watanzania leo wanajivunia amani.

Pamoja na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, Rais Malinzi Dkt Magufuli amewapa pole wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi, akisema ni kielelezo cha kiongozi aliyetukuka.


“Kabla ya Uhuru Mzee wetu, Mzee Kahama alikuwa kiongozi shupavu na mzalendo, alama ambayo ametuachia sisi Watanzania leo hii tunajivunia amani,” alisema Rais Malinzi.

Rais Malinzi ambaye katika vikao vyake vya jana hapa Dar es Salaam, alikuwa akitoa nafasi ya kumkumbuka Sir George, akisema msiba huo pia ni wa TFF kwa kuwa mmoja wa watoto wake, Joseph ni Mjumbe wa Mfuko wa Bodi ya Maendeleo ya Mpira wa Miguu wa TFF.

Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.



MALINZI AWAPA MAAGIZO MAZITO MAKOCHA WAPYA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amewazawadia makocha wapya 27 waliofuzu kozi ya ukocha kwamba kila mmoja mmoja atampa koni 20 na vizibao 22 kwa ajili ya mazoezi.

Rais Malinzi alitoa ahadi hiyo wakati wa hafla ya kufunga kozi ya ukocha ngazi ya ‘Intermidiate’ kwa makocha waliohitimu. Rais Malinzi alialikwa na waratibu kuwa mgeni rasmi ambaye awali, alishangazwa kwa namna ilivyoratibiwa kwa kufuata miongozi ya TFF na CAF.

Katika hotuba yake, Rais Malinzi aliwataka waamuzi hao kuzingatia weledi wakiwa ni mabalozi wa kupinga matumizi ya dawa za kulevya lakini zaidi wajiepushe kwa njia yoyote  ile kupanga matokeo.

Rais Malinzi alifurahishwa na idadi kubwa ya makocha waliohitimu kwani kabla walikuwa ni wachezaji wa timu kubwa na kongwe mbalimbali, “Hilo sasa linanisukuma kuwapa kila mmoja wenu koni 20 na bips (vizibao) 22,” alisema Rais Malinzi.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuwaombea dunia Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Chilla Tenga ambaye anawania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa FIFA kwa nchi zinazozungumza Kiingereza ambako anapambana na Kwesi wa Ghana.

Pia katika mkutano huo Mkuu wa CAF utakaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia ukihusisha nchi 53 kati ya 54 wanachama wa CAF, pia watapiga kura kuichagua Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa shirikisho hilo.

Kozi hiyo iliendeshwa na Wilfred Kidao - Mkufunzi anayetambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), akisaidiwa na Manyika Peter aliyefundisha programu au mtaala kwa makocha wa makipa; Dk. Nassoro Ally Matunzya aliyewanoa makocha hao kuhusu tiba za wanamichezo/wanasoka na Mkufunzi wa muda mrefu wa soka, Hemed Mteza.

Wahitimu wa kozi hiyo walikuwa Doris Malyaga ambaye ni Mwanamke pekee kati ya wanafunzi 27 walisoma kozi hiyo kwa kipindi cha siku 14 cha mwanzo wa mwaka. Doris ni mwanahabari za michezo aliyehudhuria kozi hiyo. Anaandikia gazeti la MwanaSPOTI linalotolewa na Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi (MCL).

Wengine ni nyota wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ waliopata kuchezea klabu kongwe na kubwa nchini. Wanafunzi hao ni Boniface Pawasa, Fred Mbuna, Innocent Haule, Herry Morris, Ivo Mapunda, Nizar Khalfan na Mussa Hassan Mgosi.

Wengine ni Omar Kapilima, Amosi Mgisa, Uhuru Mwambungu, Yussuf Macho, George Minja, Haruna Adolf, Selemani Omari, Ally Ruvu, Masoud Selemani, Haji Mustapha, Mhasham Khatib, Issa Ndunje, Salum Kapilima, Said Salum, Julio Elieza, Hassan Mwakami, Rajab Mponda, Ally Mbonde na Evod Mchemba.

MAYANGA ATANGAZA KIKOSI CHA TAIFA STARS

Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga leo Jumatatu Machi 13, 2017 ametangaza majina ya wachezaji 26 watakaounda kikosi hicho.

Taifa Stars, inatarajiwa kucheza na Botswana Machi 25, 2017 kabla ya kuivaa Burundi Machi 28, mwaka huu katika michezo kirafiki wakati huu wa Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika leo Makao Makuu ya TFF, yalioko Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, Mayanga aliwataja wachezaji hao kuwa ni walinda milango, Aishi Manula  (Azam FC), Deogratius Munishi (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia aliwataja Shomari Kapombe    (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael (Azam FC).

Mayanga aliwataja walinzi wa kati Vicent Andrew (Yanga SC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Erasto Nyoni   (Azam FC) ilihali aliwataja viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao     (Azam FC) na Jonas Mkude (Simba SC).

Kadhalika wako viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla  (Simba SC), Frank Domoyo (Azam FC) na Muzamil Yassin (Simba) wakati viungo wa kulia waliotajwa ni Simon Msuva (Yanga SC) na Shizza Kichuya    (Simba SC).

Viungo wa kushoto ni Farid Mussa (Teneriffe, Hispania) na Hassan Kabunda (Mwadui FC) wakati washambuliaji ni Mbwana Samatta      (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu      na AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu(Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting).

Pia Mayanga aliwataja wasaidizi wake kuwa Kocha Wa Makipa, Patrick Mwangata wakati Meneja wa timu upande wa ufundi atakuwa mwenyewe Mayanga na upande wa mipango mingine atakuwa Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu wakati Daktari wa timuatakuwa Richard Yomba huku Daktari wa viungo   akiwa ni Gilbert Kigadya.

Timu hiyo itaingia kambini Machi 19, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam na mara baada ya michezo hiyo kambi itaahirishwa Machi 29, mwaka huu.


SERENGETI BOYS WAANZA KAMBI

Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya vijana wenye umri wa miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys imeanza mazoezi rasmi leo Machi 12, 2017 kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys itakuwa kambini Dar es Salaam hadi Machi 26, mwaka huu ambako itakwenda Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa kujiandaa na michuano Afrika ambayo sasa itaanza Mei 14, 2017 badala ya Mei 21, mwaka huu.

Michezo ya kirafiki ya kimataifa itakuwa ni dhidi ya timu za vijana za Rwanda (Machi 28, 2017), Burundi (Machi 30, mwaka huu) na Uganda Aprili 2, mwaka huu). Michezo yote itafanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.

Timu hiyo itarejea tena Dar es Salaam Aprili 3, mwaka huu ambako siku inayofuata itaagwa kwa kupewa bendera na mmoja wa viongozi wa nchi kabla ya kusafiri Aprili 5, mwaka huu kwenda Morocco kwa ajili ya kambi.

Timu hiyo itaunganisha kwenda Cameroon Mei mosi, mwaka huu ambako Mei 3, 2017 itacheza mechi ya kwanza na Cameroon kabla ya kurudiana Mei 6, mwaka huu na siku inayofuata itakwenda Gabon.

Serengeti Boys ni timu ya vijana ambayo imefuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu. Timu hiyo imepangwa Kundi ‘B’ pamoja na mabingwa watetezi Mali, Niger na Angola. Ina lalengo ya kurejea na Kombe la Afrika kwa vijana.

La ikitokea imekosa nafasi hiyo angalau ikafika nusu fainali ambako kwa mafanikio hayo itakuwa tayari ina tiketi mkononi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia huko India, Novemba, mwaka huu.

Kikosi cha Serengeti Boys kinaundwa na Makipa:  Ramadhan Kabwili, Samwel Edward na Kelvin Kayego.

Walinzi:  Kibwana Ally Shomari, Nickson Kibabage, Israel Mwenda, Dickson Job, Ally Msengi, Issa Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.

Viungo: Kelvin Nashon Naftali, Ally Ng’anzi, Mohamed Rashid, Shaaban Ada, Mathias Juan, Najim Mussa, Marco Gerald, Abdulhamis Suleiman, Saidi Mussa na Cyprian Benedictor Mtesigwa.

Washambuliaji:  Muhsin Malima Makame, Yohana Mkomola, Ibrahim Abdallah, Assad Juma na Abdul Suleiman.

Benchi la Ufundi:
Bakari Shime (Kocha Mkuu)

Oscar Mirambo (Kocha Msaidizi)

Muharami Mohamed (Kocha wa makipa)
Kim Poulsen (Mshauri wa Ufundi)
Edward Evans (Mtunza Vifaa)
Shecky Mngazija (Daktari wa timu)
Gomez Dardenne (Mtaalamu wa saikolojia)

No comments: