Kila mwaka maadhimisho haya yanakuwa na dhima maalum ambako kidunia dhima ni “Kuwa Jasiri kuleta Mabadiliko” wakati dhima ya kitaifa ni “Tanzania ya Viwanda, Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya kiuchumi”. Sambamba na dhima hizi sisi kama taasisi zinazohusika na masuala ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia nchini, tunaamini kwamba ukatili wa kijinsia ni moja ya vikwazo vikubwa kwa wanawake vinavyowakwamisha kuchangia kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo kushika nafasi za maamuzi na kumiliki rasilimali. Ukatili wa Kijinsia hauwezi kuisha bila madadiliko makubwa katika maisha yetu ya kila siku, mila na tamaduni zetu pamoja na sera na sheria zetu. Ni kwa muktadha huo tumekuja na kauli mbiu isemayoni, “Kuwa Jasiri, Pinga Ukatili Dhidi ya Wanawake”.
Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha jamii, serikali na makundi mbalimbali na mtu mmoja kuchukua hatua katika kuzuia na kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake. Ikumbukwe kuwa wanawake ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya watanzania wote, wamekuwa wakikosa nafasi na sauti ya kufanya maamuzi kutokana na mifumo kandamizi kwenye jamii zetu ukiwemo mfumo dume. Tunaamini na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kusimama kwenye nafasi zao kupinga aina zote za ukatili kwa wanawake na watoto wa kike ikiwemo ndoa za utotoni ambazo bado ni changamoto na zimeongezeka kwa 4% kutoka 23% 2010 mpaka 27% 2015, huku wasichana 36 kati ya 100 wakipata mimba katika umri mdogo, rushwa ya ngono na aina nyingine za ukatili ambazo zinamzuia mwanamke na mtoto wa kike kufikia ukombozi wa kiuchumi.
Ni dhahiri kwamba suala la kupinga ukatili wa kijinsia linahusisha rasilimali kwa kiasi kikubwa. Pamoja na juhudi za serikali kuandaa na kuzindua Mkakati wa kitaifa wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mnamo mwezi Disemba mwaka 2016, tunatoa wito kwa watendaji hususan ngazi ya Halmashauri kuhakikisha fedha zinatengwa na kuelekezwa katika kutekeleza mkakati huo kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Fedha Mh. Philp Mpango wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati huo.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa kwa mwaka huu yatafanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga vilivyopo Temeke kwa kukusanyika katika viwanja hivyo kuanzia saa 1:30 asubuhi na kisha kufuatiwa na maandamano mafupi ya amani yatakayofanyika katika viwanja hivyo hivyo vya Mwembe Yanga. Mkusanyiko huo utahusisha wimbo mfupi na ugawaji wa vipeperushi kwa washiriki watakaohudhuria. Mgeni rasmi katika shughuli hii anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Tunachukua fursa hii kuwapongeza wanawake wote Tanzania na kuwatia moyo katika kupigania haki na usawa wa wanawake.
No comments:
Post a Comment