Sunday, March 5, 2017

NECTA YAENDELEA KUWATANGAZIA WANANCHI KUTOA TAARIFA ZA WATU WANAOTUMIA VYETI VYA WATU WENGINE



Na Eleuteri Mangi, MAELEZO
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) linaendelea kuwatangazia wananchi kuendelea kuwapa ushirikiano kwa kutoa taarifa mbalimbli ikiwemo taarifa kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti vya watu wengine.

Tangazo hilo limetolewa na NECTA kupitia mtandao wake www.necta.go.tz hatua ambayo inaendeleza juhudi za kuwafichua watumishi ambao wanatumia vyeti ambavyo sio vyao.

Kwa mujibu wa tangazo hilo NECTA imewataka wananchi wenye malalamiko au taarifa kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti vya watu wengine kuwasiliana nao kupitia barua pepe esnecta@necta.go.tz au simu namba +255 742 484 955.

Wananchi wametakiwa kufikisha malalamiko au taarifa hizo kwa kuzingatia muda wa saa za kazi kuanzia saa 2:30 Asubuhi hadi 10:30 jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.

Aidha, tangazo hilo limesisitiza kuwa kwa msaada zaidi wananchi wawasiliane nao kupitia barua pepe helpdesk@necta.go.tz au simu namba 0658 116 644kwa saa za kazi.

Tangazo hilo linaendelea kutoa msisitizo kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa kwa Wakuu wa Mikoa Machi 15, 2016 la kuhakiki watumishi wa Umma na kuwaondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo kwa Serikali yake.

No comments: