Siku ya Mtoto wa Afrika: Changamoto zinazowakabili Watoto Tanzania
Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu kinaungana na jamii ya ulimwengu kuadhimisha siku ya mtoto wa
Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 tangu ilipoainishwa rasmi na Junuiya ya
Umoja wa Afrika mwaka 1991.
Katika kuadhimisha
siku hii yenye kauli mbiu inayosema “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi
na Fursa Sawa kwa Watoto” Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia Ripoti
ya Haki za Binadamu 2016 kimebaini changamoto lukuki ambazo zinadumaza ustawi
wa watoto nchini Tanzania. Changamoto hizo ni pamoja na:
- Kuongezeka kwa
vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto ambapo vitendo zaidi ya 2,
571 vya ubakaji na ulawiti vimeripotiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka
2016.
- Vitendo vya
Ukatili wa kingono kufanywa na watu wa karibu kwa watoto; asilimia 49 ya
vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto vimeripotiwa kutekelezwa na
ndugu wa karibu kwa watoto hivyo kupelekea ugumu katika kufuatwa kwa sheria
kwani masuluhisho mengi huishia katika ngazi ya familia na wakati mwingine
jamii hushindwa kutoa ushahidi kwa kuoneana aibu.
- Kuendelea
kushamiri kwa ndoa za utotoni; watoto wawili (2) kati ya watano (5)
huolewa chini ya miaka 18 na kupelekea kukatisha haki yao ya kupata elimu.
- Mimba za
utotoni/mashuleni: Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu
Duniani (UNFPA) juu ya ongezeko la mimba za utotoni barani Afrika imeitaja
Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa mimba za utotoni barani Afrika.
- Vitendo vya
kikatili na mateso dhidi ya watoto: kupitia vyombo vya habari vitendo
vingi vya kikatili ikiwemo adhabu kali na zinazotweza utu wa mtoto
vimeripotiwa. Vitendo vya watoto kuunguzwa kwa moto, kupigwa hadi
kupelekea majeraha hata kujeruhiwa kwa visu au mapanga vimezidi kuripotiwa
kwa kiasi kikubwa.
- Ukeketaji: Mbali
na takwimu kuonyesha kupungua kwa vitendo vya ukeketaji, bado mila hii
potofu imeendelea kurudisha nyuma harakati za kumkomboa mtoto wa kike
kutoka katika wimbi la mila potofu.
- Vikwazo katika utekelezaji wa Sera ya
Elimu Bure: changamoto kadhaa katika utekelezaji wa sera ya elimu
bure/elimu bila malipo kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014
ikijumuisha shule nyingi zilizidiwa na wanafunzi ukilinganisha na uwepo wa
madarasa, upungufu wa walimu na vifaa vya kufundishia vimeendelea kukwaza
haki ya watoto kupata elimu bora.
- Huduma hafifu za
afya: changamoto katika sekta ya huduma za afya ikiwemo upungufu wa
asilimia 51 wa wahudumu wa afya, kukosekana kwa madawa na vifaa tiba
kumeendelea kuyumbisha ustawi wa watoto.
Sababu kuu ya kuzidi
kuongezeka kwa changamoto hizo ni pamoja na sheria kandamizi kama sheria ya
ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu msichana kuolewa akiwa na umri chini ya miaka
18; serikali kutenga bajeti duni kwenye huduma za kijamii ikiwemo afya na
elimu; umasikini; mila potofu; Imani za kishirikina; uendeshaji mashitaka
kucheleweshwa katika vyombo vya utoaji haki; malezi duni kwa watoto; rushwa
pamoja na familia na ndugu wa wahanga kujaribu kuficha aibu ndani ya familia.
Kituo chja Sheria na
Haki za Binadamu kinapendekeza yafuatayo katika kudumisha ustawi wa watoto
nchini Tanzania:
- Watanzania kwa
ujumla kutambua umuhimu wa kuzingatia haki za mtoto kwa kutowaficha
wahalifu wa vitendo vya kikatili dhidi ya watoto na badala yake kuwaibua
na kuacha sheria kuchukua mkondo.
- Wazazi na walezi
kudumisha malezi bora kwa watoto ili kuzuia mmomonyoko wa maadili
unaopelekea mmomonyoko wa ustawi kwa watoto.
- Jamii kuachana na
mila potofu pamoja na Imani za kishirikina zinazokandamiza ustawi wa watoto.
- Vyombo vya
usimamizi wa sheria ikijumuisha jeshi la polisi na mahakama kuzingatia
ustawi wa watoto wakati wa maamuzi na usimamizi wa haki.
- Serikali kufanyia
marekebisho sheria zote zinazokandamiza ustawi wa watoto ikiwemo sheria ya
ndoa yam waka 1971.
- Serikali
kuboresha sera ya elimu kuwezesha watoto wa kike kuweza kuendelea na
masomo baada ya kujifungua.
- Serikali
kuelekeza nguvu katika kuboresha huduma za kijamii na miundombinu ili
kumaliza changamoto zinazowakabili watoto hususani maeneo ya vijijini.
Mwisho, Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu kinaamini watoto ni hazina ya taifa lolote lenye
dira ya maendeleo hivyo ni wajibu wa kila mmoja kudumisha ulinzi kwa watoto.
Imetolewa Ijumaa, Juni 16 2017
Bi. Anna Henga
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
No comments:
Post a Comment