HALI
YA KILIMO NCHINI
Serikali yeyote
makini lazima ihangaike na masuala yanayowahusu wananchi wake walio wengi, na
hapa Tanzania watu hao (walio wengi) ni Wakulima. Hivyo basi, kipimo kikuu cha
kuondoa umasikini wa Watanzania ni kuondoa umasikini wa wakulima.
Tanzania imeendelea
kutegemea Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake
kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65.5 ya Watanzania na inachangia zaidi ya
asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye miaka yenye mvua za
kutosha. Katika mwaka 2016 Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 29.1 ya Pato la
Taifa ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2015. Mchango mkubwa katika Pato la
Taifa ulitokana na Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine za kiuchumi.
Kwa kuwa asilimia
kubwa ya Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, hivyo kilimo
kinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kupunguza umaskini. Hivyo
basi, unapowekeza kwenye sekta ya kilimo unawekeza kwa theluthi mbili ya
watanzania. Unapokuza kilimo unakuza uchumi wa theluthi mbili ya watanzania, na
unapoacha kilimo kishuke maana yake umewafukarisha theluthi mbili ya
Watanzania.
Kwa mujibu wa
wataalamu wa Uchumi, ili kupunguza umasikini Tanzania kwa kiwango kikubwa,
sekta ya kilimo inapaswa kukua kwa asilimia zaidi ya 8% angalau kwa miaka
mitatu mfululizo, na ukuaji huo uendelee kukua kwa wastani wa 6% kwa muda miaka
kumi mfululizo.
Hali ikoje nchini?
Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wakati
akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa
2017/18, kwa miaka hii mitatu mfululizo ukuaji wa Kilimo umekuwa ukishuka
nchini (Na hivyo ukuaji zaidi wa umasikini). Mwaka 2014 sekta ya Kilimo ilikua
kwa 3.4%, Mwaka 2015 Kwa 2.3% na Mwaka 2016 Kwa 2.1%.
Taarifa ya ya robo
mwaka ya Benki Kuu nchini (BOT quarterly economic bulletin) inayoishia Disemba
2016 inaonyesha tofauti na anachosema Waziri katika hotuba yake hiyo ya bajeti.
Kwa mujibu wa tarifa ya BOT ni kuwa sekta ya Kilimo ilikua kwa kasi ya 0.6% tu
kutoka ukuaji wa 2.3%. 65.5% ya Watanzania wote wamejiajiri katika sekta ya
Kilimo, hivyo mdororo huu ya sekta ya Kilimo kutoka ukuaji wa 2.5% mpaka ukuaji
wa 0.6% ni ishara mbaya mno kwa ustawi wa zaidi ya robo tatu ya Watanzania.
Kwa Vijijini 78% ya
Watanzania wanajihusisha na Kilimo. Hii maana yake ni kwamba wananchi wengi
vijijini hawafanyi uzalishaji, jambo hili ni hatari sana, ni dalili kuwa
ufukara wa watu wetu unazidi. Ni kwa sababu hii, pamoja na uchumi wetu kukua
kitakwimu, 7% kwa mwaka kama tunavyoambiwa, lakini bado wananchi wetu walio
wengi wanaishi kwenye dimbwi la ufukara, maana msingi (base) ya ukuaji huo wa
Uchumi hauhusishi kilimo, hauhusishi zaidi ya robo 3 ya Watanzania.
Tunajenga uchumi
unaowaacha pembeni zaidi ya theluthi 2 ya watanzania wote. Ukuaji huu mdogo wa
Kilimo unapaswa kuishtua Serikali kwani ni hatari sana, ni hatari mno. Maana
unajenga uchumi unaowaacha karibu zaidi ya robo 3 ya Watanzania kwenye ufukara
huko vijijini, ni uchumi unaopanua matabaka ya mafukara na matajiri. Ndio
msingi wa umasikini wa wananchi wetu miaka 50 baada ya Uhuru wetu.
Tatizo
hasa ni nini? Kwanini ukuaji wa kilimo unashuka na
hivyo umasikini wa Watanzania kuzidi? Tatizo kubwa ni sera za Serikali pamoja
na utekelezaji wake. Serikali haiwekezi vya kutosha kwenye kilimo, Na hata
ikipanga mipango juu ya kilimo haitekelezi kabisa mipango husika au haitekelezi
kwa wakati, kiasi matokeo yenye tija yanayotarajiwa hayapatikani kabisa. Tatizo
hilo ndio mzizi mkubwa kwenye sekta nzima ya kilimo nchini, na hata kwenye hili
sakata la hali mbaya ya pembejeo katika mikoa mitano inayolima korosho zaidi
nchini.
Katika bajeti ya
mwaka 2015/16, bajeti ya mbolea ya Ruzuku katika Wizara hii ilikuwa ni shilingi
bilioni 78. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya tano ilishusha fedha za
ruzuku ya mbolea mpaka Shilingi bilioni 10 katika mwaka wa Fedha wa 2016/17.
Hii ilikuwa ishara ya dhahiri ya kukipuuza kilimo, kuwapuuza 65.5% ya
Watanzania wote, kutokujali chanzo cha 100% ya chakula chote cha Watanzania,
kupuuza sekta inayochangia theluthi moja ya uchumi wa Taifa. Si hivyo tu, katika
bajeti ya mwaka 2016/17, bunge liliidhinishia Wizara hii fedha za miradi ya
maendeleo katika kilimo, kiasi cha bilioni 100.53. Waziri alilieleza bunge hapa
kuwa mpaka Mei 4, 2017, Wizara imepokea shilingi bilioni 3.34, sawa 3.31% ya
fedha zote za maendeleo ya kilimo. Jambo hili linasikitisha mno, ni jambo
linaonyesha kuwa hatuwajali wanyonge wa Taifa hili.
Kwetu sisi ACT
Wazalendo tunaofuata Ujamaa wa Kidemokrasia, Kilimo ndio sekta ya msingi, ndio
uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, ni sekta nyeti ambayo hatutaacha kuisemea,
ndio msingi wa waraka huu.
HALI
YA UZALISHAJI WA KOROSHO NCHINI PAMOJA NA MCHANGO WA ZAO HILI KATIKA UCHUMI WA
TAIFA
katika msimu wa mwaka
2016/2017 uzalishaji wa mazao makuu ya asili ya biashara ambayo ni Korosho,
Miwa ya Sukari, Pamba, Mkonge, Kahawa, Chai, Tumbaku na Pareto umepungua na
kuongezeka kwa viwango tofauti ingawa uzalishaji wa jumla kwa mazao hayo
umeongezeka kufikia tani 881,583, ikilinganishwa na tani 796,502 mwaka
2015/2016. Uzalishaji unaoendelea kwa mwaka 2016/2017 na matarajio kwa mwaka
2017/2018 ni kuzalisha jumla ya tani 953,825 ya mazao hayo kama ilivyooneshwa
katika Jedwali Na. 1.
Uzalishaji wa mazao
ya Korosho, Sukari na Pareto umeongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo
bei nzuri katika zao la Korosho kutokana na Mfumo wa Stakabadhi Ghalani,
Ushiriki wa Wanunuzi kutoka nchi za China na Vietnam, pamoja na hamasa
iliyotokana na ongezeko la bei. Kwa Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) za
mwezi Februari mwaka 2017, zao Korosho lililiingizia Taifa fedha za Kigeni, Dola
za Kimarekani, milioni 346.6, ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka
2016, ambapo tulipata Dola za Kimarekani milioni 184.9, kiasi hicho kinalifanya
zao la korosho kuwa zao namba 1 la kuingiza fedha nyingi za kigeni hapa nchini
kwetu.
Jedwali
Na. 1 Uzalishaji wa Mazao ya Asili ya Biashara (Tani) kati ya 2015/2016 na
2017/2017 na matarajio kwa mwaka 2017/2018.
Zao
|
2015/2016
|
2016/2017
|
2017/2018
|
Pamba
|
|
122,000
|
150,000
|
Chai
|
32,629
|
31,000
|
35,000
|
Pareto
|
2,011
|
2,500
|
2,600
|
Korosho
|
155,416
|
260,000
|
300,000
|
Mkonge
|
42,314
|
42,000
|
43,000
|
Sukari
|
293,075
|
329,840
|
324,325
|
Kahawa
|
60,921
|
47,999
|
43,000
|
Tumbaku
|
60,691
|
60,691
|
55,900
|
Jumla
|
796,502
|
881,583
|
953,825
|
Ukizitazama takwimu
zote hizi kwa undani, utagundua kuwa msimu wa korosho ulioshia Februari mwaka
huu katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga ndio msimu bora zaidi
kuliko yote kwa wakulima tangu tuanze kulima zao hilo nchini. Hiyo ni kwa
sababu, kwanza uzalishaji uliongezeka kwa zaidi ya tani 100,000, pili bei ya
korosho kupaa kwa zaidi ya mara mbili, bei ya zao hilo ilipanda hadi kati ya
Sh3,700 na Sh4,000 kwa kilo, wakati bei elekezi ya msimu iliyokuwa imepitishwa
na kikao cha wadau waliokutana Bagamoyo ilikuwa Shilingi 1,300. Miaka ya nyuma
wakulima wamekuwa wakiuza korosho zao kwa wastani wa wa Sh1,200 kwa kilo. Uchambuzi
wa takwimu uliofanywa na ACT Wazalendo katika minada 10 ya awali iliyokuwa
chini ya chama kikuu cha ushirika cha Mtwara na Masasi (Mamcu), unaonyesha kuwa
bei ya chini ilikuwa ni Shilingi 2,610 kwa kilo ambayo bado ni kubwa mara mbili
ya bei elekezi.
Sababu
kuu ya kupanda kwa uzalishaji wa zao la korosho nchini
ni kutokana na wakulima kuandaa mashamba yao vizuri, kupiga dawa kwa wakati na hivyo kupata korosho bora kuliko
zilizopatikana katika nchi nyingine kama Msumbiji na nyingine za Afrika
Magharibi.
Sababu
kuu ya kupaa kwa bei ya korosho nchini ni mabadiliko
mbalimbali ya kiuzalishaji na kisoko ndani na nje ya nchi, hususan kuporomoka
kwa uzalishaji katika nchi maarufu kwa zao hilo kama Vietnam (inayozalisha 58%
ya korosho zote duniani). Uzalishaji wa Vietnam ulipungua kwa asilimia 11 mwaka
jana kutokana na ukame, huku mahitaji yake yakiongezeka kwa asilimia 53 tangu
2010. Hivyo haikushangaza kwa mara ya kwanza katika historia ya soko la korosho
nchini, kushuhudia ushiriki mkubwa wa wazabuni kutoka nchi za China, Singapore
na Vietnam tofauti na wazabuni wa kawaida tu kutoka nchini India.
Katika kanuni za
biashara, kwa kuongezeka kiwango cha uzalishaji wa korosho nchini kama
ilivyokuwa mwaka huu, ilitarajiwa kuwa bei yake ingeshuka zaidi, lakini hapa
nchini bei imeongezeka kwa sababu mahitaji ya zao hilo kwenye soko la dunia
yalikuwa ni makubwa mno tofauti na uzalishaji wake mdogo. Hivyo utaona kuwa
hali ya bei hii kubwa ya korosho nchini, ilitokana na kiasi kikubwa na kuanguka
kwa uzalishaji wa zao hilo katika nchi zinazoongoza kama Vietnam.
Sababu nyengine ni
udhibiti wa soko wa wakulima kwa kuzuia unyonyaji uliotokana na utaratibu wa
uuzwaji holela wa korosho (Kangomba), korosho yote kuuzwa kwa pamoja na kwa
uwazi, kwa matakwa ya wakulima ambao wanashirikishwa kuteua mzabuni mwenye bei
nzuri kwenye mnada, pamoja na mfumo mpya wa mauzo ya korosho kwa kuendesha
minada kila wilaya.
TAARIFA
JUU YA HALI YA UPATIKANAJI, USAMBAZAJI NA UGAWAJI WA PEMBEJEO KWA WAKULIMA WA
KOROSHO NCHINI
Ongezeko hili la bei ya
zao la korosho limeongeza umuhimu wa zao hili kwa wakulima, kama mkombozi wa
kuwaondoa kwenye umasikini, na limeleta hamasa kubwa kwenye mikoa hii mitano inayozalisha
korosho zaidi nchini, hasa kwa mikoa ya kusini ambapo korosho ndio zao kuu la
kilimo pia. Mashamba yaliyotelekezwa yamefufuliwa, vichaka vimefyekwa na
mikorosho imepaliliwa. Hata mikoa ambayo kijadi haikuzalisha korosho kama vile
Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Njombe na Morogoro nayo imechangamkia fursa
hii na kuanza kupanda miche ya korosho.
Pamoja na umuhimu wa zao
la korosho kwa uchumi wa nchi, na kwa wakulima wote wa korosho nchini, bado Serikali
haijaweka mkazo wa kutosha kuhakikisha zao hili linawaondolea umasikini
wananchi, badala yake imekuwa kikwazo cha kuondoa umasikini huo wa wananchi.
Tutaeleza.
Tanzania ni nchi
mojawapo Barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara yenye matumizi ya chini sana ya mbolea katika ngazi ya wakulima wadogo
(smallholder farmers). Kwa sasa Tanzania imefikia kiwango cha kilo 19 tu za
virutubisho kwa hekta, yakiwa ni matumizi madogo mno kwa viwango vya dunia,
mfano nchi ya China ina wastani wa matumizi ya kilo 210 kwa hekta moja.
Matumizi
hayo yetu ya mbolea na virutubisho pia ni kiwango cha
chini hata kwa viwango vya Kiafrika. Azimio la Maputo (The Maputo Declaration,
2003) liliazimia masuala mbalimbali katika kilimo, pamoja na mambo mengine; liliweka
sharti la kuongeza matumizi ya mbolea katika eneo la ukanda wa SADC kufikia
angalau kilo 50 za virutubisho kwa hekta.
Moja
ya matatizo makubwa ya uzalishaji wa zao la korosho
ni ugonjwa wa ubwiri unga. Ugonjwa huu unasababishwa na vimelea aina ya uyoga
(fungus) viitwavyo Oidium anacardii. Ugonjwa huu ni hatari sana, kiasi
kwamba kama haukuthibitiwa, unaweza kupunguza mavuno kwa zaidi ya asilimia 70,
ugonjwa huu umeenea katika mikoa yote inayolima zao hili Tanzania. Hapo awali
ugonjwa huu ulikuwa unaitwa kwa jina la “ukungu” kutokana na uhusiano wake
mkubwa na hali ya hewa ya ukungu (litabwe kwa Kimakonde) unaoonekana
alfajiri/asubuhi katika miezi ya Juni - Septemba. Hivyo basi, jina la Ubwiri
unga linatumika sasa ili kuwawezesha wakulima wasichanganye vitu hivyo viwili.
Ugonjwa
huu unashambulia maeneo yote machanga na teketeke
katika mti wa mkorosho, hasa machipukizi, majani, maua, mabibo na korosho
changa (tegu). Athari kubwa ya ugonjwa huu inatokana na mashambulizi ya maua,
ambayo hushindwa kufunguka na kuwezesha chavua kufanya kazi yake, hatimaye
hunyauka na kukauka.
Dawa ya Salfa
(Sulphur) ndiyo dawa inayotumika kwa wingi zaidi kukinga
ugonjwa wa ubwiri unga. Dawa hii ambayo ni ya unga, inapulizwa kwa
kutumia mashine maalumu (motorized blower) ya kupulizia dawa km.
Maruyama. Kiwango cha gramu 250 kwa mti, kwa mzunguko, ndicho kinapendekezwa.
Hivyo basi kwa mizunguko mitano kiasi cha kilo 1.25 cha salfa kwa mti
kwa mwaka kinahitajika.
Wakati sahihi wa
kuanza upuliziaji unaanza pale ambapo karibu asilimia 20
za maua yamejitokeza na wakati zaidi ya asilimia 5 ya maua hayo
tayari yawe yanaonyesha dalili za ugonjwa.
Sababu
kuu ya kupanda kwa uzalishaji wa zao la korosho nchini
kwa msimu uliopita ni kutokana na wakulima kuandaa mashamba yao vizuri, kupiga
dawa ya Salfa kwa wakati na hivyo kupata korosho bora kuliko zilizopatikana
katika nchi nyingine kama Msumbiji na nyingine za Afrika Magharibi. Serikali
yetu inataka kuua uzalishaji huu mkubwa wa wakulima wetu.
Nini
Kimetokea? Mwezi Mei mwaka huu, kwenye kikao cha mwaka cha
wadau wa zao la korosho kilichofanyika mjini Dodoma, Serikali ilitangaza uamuzi
wa kugawa pembejeo bure kwa wakulima wote wa zao la korosho. Uamuzi huo
ulitangazwa na waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, ndugu Charles Tizeba
mbele ya Waziri Mkuu, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo. Kutangazwa
kwa uamuzi huu kuliibua shangwe kubwa kwa wakulima wa korosho ambao walifurahia
kupunguziwa mzigo wa kununua pembejeo.
Uamuzi huu ulileta
matokeo yafuatayo:
- Mfumo wa
Pembejeo ya ruzuku ulifutwa.
Kabla
ya mfumo wa kugawa pembejeo bure kutangazwa, kulikuwa na mfumo wa pembejeo
uliokuwa ukiendeshwa na Vyama vya Msingi vya ushirika (Amcos). Vyama hivi vya
msingi vya ushirika vilikuwa vinakusanya fedha kwa wakulima wakati wa mauzo (kiasi
cha shilingi 15,000 tu kwa mfuko), kununua pembejeo nje ya nchi na kugawa kwa
wakulima.
- AMCOS
Walirudisha Fedha za Wakulima
Kabla
ya kutangazwa kwa uamuzi huu, vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vilikuwa
vimeshakusanya fedha kwa wakulima na vinajipanga kununua Salfa nje ya nchi. Kwa
uamuzi huu wa serikali, vyama vya ushirika viliamriwa kuwarudishia wakulima
fedha zilizokusanywa kwa sababu “Pembejeo ya bure” ingeletwa.
- Wakulima
Walizitumia Fedha Zilizorejeshwa Kutoka Amcos
Baada
ya wakulima kurejeshewa fedha zao kutoka kwa vyama vyao vya msingi vya ushirika
(Amcos), wengi wao walizitumia fedha hizo kwa matumizi mengine kwa kuwa
walikuwa na uhakika wa kupata pembejeo ya bure kutoka serikalini.
- Waagizaji
Binafsi “Waliufyata”
Mbali
na vyama vya ushirika, pembejeo huuzwa pia kwenye soko na wafanyabiashara
binafsi. Kwa msimu wa mwaka 2016/2017, pembejeo aina ya Salfa, ambayo ndiyo
maarufu zaidi, iliuzwa kati ya shilingi 3000 - 35,000 kwa mfuko mmoja, na
wauzaji binafsi. Kutangazwa kwa ujio wa Salfa ya bure kuliwafanya
wafanyabiashara wengi binafsi kukhofia kukosa soko la Salfa na pembejeo
nyingine muhimu walizoagiza na hivyo kupata hasara.
Kinyume na ahadi ya
serikali ya kuleta pembejeo ya bure, ya kutosha na kwa wakati, hali imekuwa
tofauti mno. Matatizo makubwa yametokea kama ifuatavyo;
- Pembejeo Hazikuletwa
kwa Wakati
Kwa
mfano katika Wilaya ya Nachingwea, Mkoani Lindi, ambayo iliongoza kwa
uzalishaji wa korosho katika msimu uliopita kwa kuzalisha tani 20,000 huwa inapofikia
mwezi Mei kila mwaka wanakuwa wameanza kupuliza dawa hizo. Lakini mpaka mwezi
wa Juni mwishoni pembejeo husika hazikuwa zimefika. Hali hiyo iko hivyo kwa
mikoa yote mitano.
Watafiti
wa Chama chetu waliojikita kwenye wilaya hii kwa sababu ndiyo wilaya iliyoongoza
kwa uzalishaji, walizungumza na wananchi, wakulima, viongozi wa vyama vya
msingi vya ushirika ambao kwa undani walielezea hali ilivyo na kuitupia lawama
serikali kwa ucheleweshaji huo wa pembejeo.
Maelezo
haya ya wakulima kwa watafiti wetu hayakuwa tofauti na maelezo waliyoyatoa
mbele ya viongozi wa serikali. Mfano, Juni 22, 2017 wakizungumza kwenye mkutano
wa hadhara, mbele ya mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango, uliofanyika
katika kijiji cha Mpiruka A, mkutano ambao viongozi wa ACT Wazalendo
walihudhuria, wakulima hawa walionyesha kukatishwa tamaa na uchelewehwaji wa
pembejeo, na matumaini yao ya uzalishaji mkubwa kama msimu uliopita yameanza
kufifia kabisa.
- Pembejeo
Zilizoletwa ni Kiduchu Mno.
Hata
baada ya pembejeo hizo kuletwa, mwezi huu (Julai) mwanzoni, bado kasma
iliyopelekwa haikidhi haja na mahitaji yaliyopo, maana ni ndogo mno. Kwa mfano,
Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma, yenye mahitaji ya tani 5,000 za Salfa kwa
msimu huu wa uzalishaji, imepewa mgao wa tani 1000 tu Salfa, ambayo ni 20% ya
mahitaji yote.
Mfano
mwengine ni Wilaya ya Nachingwea, wilaya iliyoongoza kwa uzalishaji wa korosho
nchini katika msimu uliopita, kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya hiyo, mahitaji
halisi ya dawa ya Salfa ya unga ni tani 20,000. Hata hivyo mgao ulitolewa na bodi
ya korosho ni tani 1300 tu, ikiwa ni 6.5% ya mahitaji ya wilaya nzima.
Hii
imesababisha wakulima wengi kutopata kabisa Salfa, na hivyo kuwaacha bila
pembejeo kwa mikorosho yao. Hata kwa waliopatiwa Salfa, wengi wao wamepata wastani
wa mfuko mmoja unaotosha kupulizia hekari moja tuu yenye mikorosho 30 tu. Hii
ni kinyume na ahadi ya serikali kugawa Salfa, na hivyo hata kwa mkulima mdogo
tu mwenye hekari chache kutopata pembejeo za kutosha. Kinyume na ahadi ya
Serikali ya kutoa bure pembejeo za kutosha.
- Pembejeo
Zilizoletwa Kutokuwa na Ubora
Yapo
madai kutoka katika wilaya za mikoa yote mitano ambazo Viongozi na Watafiti wa
ACT Wazalendo walizungumza na wananchi, wakulima pamoja na viongozi wa vyama
vya msingi vya ushirika (Amcos) kuwa Salfa husika iliyosambazwa, pamoja na
kutofikishwa kwa wakati na kuwa kidogo mno, bado ina ubora duni kwa sababu ya
kujaa chengachenga zinazopunguza ufanisi wakati wa kupulizia.
Jedwali
Na. 2 Bei za Salfa katika baadhi ya Wilaya zinazozalisha zao la korosho zaidi
nchini.
Eneo
|
Bei ya Salfa
(Amcos)
|
Bei ya asili ya
Wafanyabiashara
|
Bei ya sasa ya
Wafanyabiashara
|
Nachingwea
|
|
30,000
|
80,000
|
Kilwa
|
15,000
|
35,000
|
Pembejeo ya Salfa haipatikani kabisa
|
Liwale
|
15,000
|
35,000
|
53,000
|
Tandahimba
|
15,000
|
35,000
|
55,000
|
Masasi
|
15,000
|
30,000
|
90,000
|
Newala
|
15,000
|
30,000
|
70,000 – 80,000
|
Tunduru
|
15,000
|
35,000
|
70000-80000
|
Mtwara Mjini
|
15,000
|
30,000
|
50,000
|
Mtwara Vijini
|
15,000
|
35,000
|
55,000
|
Ruangwa
|
15,000
|
35,000
|
60,000 – 80,000
|
Lindi Mjini
|
15,000
|
35,000
|
60,000 – 80,000
|
Lindi Vijijini
|
15,000
|
35,000
|
60,000 – 100,000
|
Nanyumbu
|
15,000
|
35,000
|
90,000
|
Ndanda
|
15,000
|
35,000
|
90,000
|
Rufiji
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
Mkinga
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
Mkuranga
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
Kisarawe
|
15,000
|
35,000
|
70,000
|
Nanyamba
|
15,000
|
35,000
|
90,000
|
Baada ya kugundua
kuwa serikali imefeli kutekeleza ahadi yake ya kugawa Salfa yenye ubora bure,
kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa, wakulima wameamua kupambana binafsi
ili kunusuru mikorosho yao, mustakabali wao na kujiepusha na kuzama kwenye
ufukara, kwa kila mmoja kwa nafasi yao kujaribu kununua Salfa kutoka kwa
wafanyabiashara binafsi. Kwa wafanyabiashara binafsi, jambo hili limegeuka
fursa kwao, baada ya kugundua kuwa Serikali imefeli katika kutimiza ahadi yake wafanyabiashara
hawa wametumia fursa hiyo kujitajirisha, kwanza kwa sababu ya uhaba wa Salfa,
pili kwa kuwa wanajua wakulima hawana njia mbadala ya kupata Salfa tofauti na
kwao wao.
Bei ya Salfa inapanda
kila uchwao kwa kasi ya roketi. Kwa mfano, kwa Wilaya ya Tunduru, kwa kipindi
cha mwezi mmoja tu wa Julai, bei ya mfuko mmoja wa Salfa imepaa kutoka 35,000
hadi 100,000 sawa na ongezeko la zaidi ya 200%. Kiwango hicho cha bei juu ya
Salfa hakijawahi kushuhudiwa tangu kilimo cha korosho kianze nchini, uzembe wa
Serikali unawaletea mateso wananchi.
Wakulima wachache
wenye akiba ya fedha wanatumia akiba yao ambayo wangeitumia kwenye shughuli za
maendeleo kununulia Salfa kwa matumaini hafifu kuwa “Dhahabu ya Kusini”
itawalipa. Wengi wanayatazama mashamba yao waliyoyapalilia kwa uchungu kwa
sababu hawana namna ya kufanya. Furaha yao ya awali ya kupata Salfa ya bure
imegeuka kilio kikuu.
Tujiulize maswali
haya:
- Je
Serikali Ilikuwa na hakika au ilikuwa inafanya mzaha na siasa tu kwa ahadi
yake hewa ya pembejeo za bure inayogharimu maisha ya wakulima?
- Je
Serikali Ilifanya uchambuzi wa kina kuhusu mahitaji halisi ya pembejeo ya
wakulima wa korosho nchini, na uwezo wa Serikali au ilikurupuka tu?
- Waziri
Mkuu, Waziri wa kilimo na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho walipohakikishia
wakulima kuwa pembejeo itapatikana kwa wingi, walimaanisha hii hii iliyokuja
kwa kuchelewa, isiyo na ubora na iliyogawiwa kwa uchache au kuna nyingine
inakuja?
- Serikali
ilipovunja mfumo wa pembejeo ya ruzuku chini ya vyama vya msingi vya ushirika
vya walikuwa na nia njema na wakulima?
Ni dhahiri kuwa
Serikali hii imeshindwa kuwajali wakulima hawa, ni dhahiri kuwa kuwa Serikali
imeshindwa kuendesha uchumi wan chi hii.
MAPENDEKEZO
YA ACT WAZALENDO
Ni dhahiri kuwa
Serikali ya CCM wameshindwa kuendesha uchumi wa Taifa, imeshindwa kutimiza
ahadi zake kwa wakuliwa wa korosho, imevunja na kuharibu mfumo imara wa
wakulima wenyewe kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu, haijui ukubwa wa
tatizo ililolitengeneza kwa kuwa haishughuliki na masuala ya wananchi bali
inashughulika na na hujuma dhidi ya vyama vya upinzani tu. Ni dhahiri kuwa hali
iliyoko sasa ikiachwa iendelee itapunguza uzalishaji wa korosho nchini,
itapunguza kipato cha wananchi, na itawadidimiza kwenye ufukara.
Kutokana na hali hiyo,
Chama cha ACT Wazalendo kinatoa wito kwa serikali ya CCM kuchukua hatua za
haraka kurekebisha mambo, ikiwemo:
HATUA
ZA DHARURA:
- Serikali ifanye
haraka kutimiza ahadi yake ya kufikisha pembejeo ya bure kwa wakulima wa
korosho, kwa kuhakikisha inafikisha kiwango cha pembejeo kinacholingana na
mahitaji yaliyoko. Taarifa juu ya mahitaji ya wakulima ziko Serikalini, ni
muhimu serikali ipeleke pembejeo kulingana na mahitaji. Serikali ichukue
hatua za dharura kuagiza pembejeo kuondosha uhaba wake.
- Serikali
inunue pembejeo zote kutoka kwa wafanyabiashara binafsi, na kuigawa bure
kwa wananchi kama ilivyoahidi wakati, au itoe ruzuku kuhakikisha kuwa
wakulima watanunua kwa bei ya Amcos ya 15,000 kwa mfuko mmoja.
- Serikali
ichukue hatua kali dhidi ya wauzaji wa pembejeo wanaopandisha bei ya pembejeo
kila siku bila huruma. Ongezeko la sasa la hadi shilling 100,000 kwa mfuko
mmoja wa Salfa halina utetezi wowote wa kibiashara zaidi ya uchu wa
kutumia uhaba wa pembejeo uliosababishwa na uzembe wa serikali
kujitajirisha.
- Serikali
ichunguze ubora wa Salfa inayogawiwa ambayo inalalamikiwa na wakulima kuwa
na ubora duni.
- Serikali
ichukue hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaolalamikiwa kuchanganya
unga wa nafaka kwenye sulphur ili kujipatia faida maradufu.
HATUA
ZA MUDA WA KATI:
- Serikali
ifanye uchambuzi wa kina wa mahitaji halisi ya kila mkulima na kuwa na
uhakika wa bejeti yake ndipo itangaze na kutekeleza mfumo wa Salfa ya
bure. Isikurupuke tu kwa lengo la kutaka sifa.
- Serikali
itoe taarifa za uhakika mapema kuhusu upatikanaji wa pembejeo badala ya
kutoa taarifa za hadaa. Kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakijinunulia
pembejeo wenyewe. Ni bora serikali ieleze wazi juu ya uwezo wake ili
wakulima waweze kujiandaa mapema kwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kununua
pembejeo.
- Iwapo
serikali serikali itakuwa haina uwezo wa kugawa Salfa yote bure, kama
ilivyoonekana, ieleze kwa undani kiwango inachoweza kutoa bure, na iimarishe
mfumo wa pembejeo kupitia Amcos kama ilivyokuwa kawaida.
HATUA
ZA MUDA MREFU:
- Kufungamanisha
sekta ya korosho na hifadhi ya jamii ili kupitia fao la bei kuweza kuweka
uimara wa bei za mazao na pembejeo. Fao la bei litalinda ustawi wa
wakulima wa korosho na kuwaepusha na hasara iwapo bei ya korosho ya msimu
huu itaanguka tofauti na msimu uliopita. Hilo litawezekana kwa kutunga
Sheria kuwezesha mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa mafao ya Bima ya Afya,
Bima za Mazao na majanga (Crop Insurance) kwa kilimo na mifugo na Fao la
Bei (Price Stabilization Benefit).
- Kuwaunganisha
wakulima wote wa korosho nchini katika hifadhi ya jamii, na hivyo kuwa na
uhakika wa akiba uzeeni kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta rasmi pamoja
na kupata faida ya Bima ya Afya, na hivyo matibabu bure yatokanyo na
mifuko ya hifadhi ya jamii. Mchango kwa watu walio nje ya sekta rasmi ni
shilingi 20,000 tu kwa mwezi.
- Kupanua
hifadhi ya jamii na kuwafikia wakulima, wafugaji na wananchi wengine
waliojiajiri kwa kutunga sheria itakayopelekea Serikali kuchangia theluthi
moja ya kila mchango wa mwananchi atakayechangia kima cha chini cha
michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa sasa mchango wa 20,000 wa
mtu asiye kwenye sekta rasmi unabaki kama ulivyo tu bila kujaliziwa.
- Serikali
ichochee Tija kwenye Kilimo cha korosho kwa kuhakikisha tunaongeza thamani
ya mazao ya korosho hapa nchini kwa kuhimiza kupunguza uuzaji wa korosho
ghafi. Jambo hilo litawezekana kwa uwekezaji mkubwa wa viwanda vya
ubanguaji wa korosho.
- Kutumia
Hifadhi ya Jamii kuwezesha wakulima kujiwekea akiba kupitia vyama vyao vya
msingi vya ushirika (Amcos) na kupata mikopo ya gharama nafuu ili
kuanzisha upanuzi wa kilimo chao, uongezaji thamani wa mazao na kupata
Bima ya Afya.
- Kutumia
Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama miundombinu ya kilimo,
viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, vyuo vya ufundi na miundombinu ya
usafirishaji mazao kama reli kwani kwa uasili wake madai dhidi ya mifuko
(liabilities) ni ya muda mrefu.
Hitimisho: Sisi kama
chama cha siasa, kwa kuzingatia falsafa ya chama chetu ya Siasa ni Maendeleo,
tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda
maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa pembejeo kwa
wakulima hawa wa korosho nchini, kuhakikisha kuwa pembejeo husika znapatikana
katika bei ambayo watanzania wanaimudu, na zinapatikana kwa wakati.
Ado Shaibu – Katibu, Kamati
ya Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi
ACT Wazalendo
Julai 30, 2017
Dar es salaam, Tanzania