Afisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni mlezi wa Kata ya Vingunguti katika masuala ya usafi Msongo Songolo amewataka wananchi wa kata hiyo mtaa wa Miembeni kuendelea kuyatunza mazingira kwa kufanya usafi kwani kufanya hivyo kuna faida kubwa ikiwemo kupunguza gharama za matibabu.
Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam katika Jumamosi ya usafi ya mwisho wa mwezi ameeleza kuwa suala la usafi hupelekea kuepuka gharama za matibabu kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, pia ili taifa liwe na watu wenye afya lazima watu wawe wasafi.
" Wananchi wanao wajibu wakufanya usafi kama wakiendelea kuwa wachafu shughuli za kiuchumi zitashindwa kufanyika"
Kwa upande wake Diwani Mwenyeji wa Kata ya Vingunguti ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Omary Kumbilamoto amepongeza wananchi kushiriki katika suala la usafi na kueleza kuwa Vingunguti ya zamani siyo ya sasa kwani hata maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu yamepungua huku ripoti zikieleza ni watu wawili tu ndiyo wameripotiwa kuugua wakati hna mahema ya wagonjwa yameondolewa Vingunguti.
Naibu Meya Kumbilamoto ameongeza kuwa wataendelea kumualika mlezi wao katika kila mtaa ili kuhamasisha suala la usafi kwa kila mwana Vingunguti.
" Leo tumeanza na Mtaa wa Miembeni kwa kumualika mlezi wetu, tutaendelea kufanya hivyo kwa mitaa mingine ili kuhakikisha tunakuwa na Vingunguti safi" Alisema Kumbilamoto
No comments:
Post a Comment