Saturday, February 17, 2018

ACT - WAZALENDO YALAANI MAUAJI YA MWANAFUNZI NIT

Chama cha Act Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa tukio la mauaji ya Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) aliyekuwa anasomea shahada ya kwanza ya Ugavi na Usafirishaji ndg. Aquilina B. Akwilia yaliyofanywa na Jeshi la polisi kama njia ya kukilinda chama cha mapinduzi kwa gharama ya uhai wa raia wasio na hatia.
Tunalaani Mauaji haya pamoja na mauaji ya Mwenyekiti wa Chadema wa kata ya Hananisifu na matumizi ya nguvu yaliyofanywa na Jeshi la polisi yaliowaacha Wananchi wengi katika majeraha. Tunasikitika kuona kwamba Nchi inayojinasibu kuwa ni ya amani Jeshi la polisi limekuwa ni wakala wa serikali iliyopo madarakani, polisi wanaovaa Sare zao zinazolipiwa kwa jasho la wanyonge wanatumika kuwakandamiza, kuwanyanyasa, kuwasukumasukuma na kuondoa uhai wa Wananchi hao. 

Tunasikitika na tunakataa kuona Tanzania inaingia katika ubaguzi wa vyama. Utu na heshima ya binadamu wa Tanzania hauwezi kupimwa na uvyama, Ccm imeamua kuasisi ukabila wa vyama ambao ni mbaya kuliko ukabila wa makabila. Kipimo cha uwezo wa kuishi hakiwezi kuwa uanachama wa vyama vya siasa. Kila mtu ana haki ya kuishi.

Pia, tunaomba viongozi wa dini na makundi mengine ya jamii kukemea na kukataa mwenedelezo huu wa mauaji unaofanya na vyombo vya dola kwa maslahi ya watu wachache wanaotaka madaraka. Tusipochukua hatua sasa CCM italiingiza taifa letu katika machafuko.

Mwisho, tunatoa wito kwa vyama vya siasa na wapenda amani wote ndani ya Nchi kukutana na  kuchukua hatua hupesi kukomesha tabia hii inayoota mizizi. Tusipo simama kidete na kupinga matukio haya, taifa litaingia kwenye machafuko na kuwa taifa lilioanguka kama ilivyo kwa mataifa mengi yenye machafuko yalivyoanguka.

Imetolewa, Leo 17 Feb 2018
Yeremia Kulwa Maganja.
Mwenyekiti, Act Wazalendo.
Kilwa Masoko, Lindi.

No comments: