Monday, April 16, 2018

TIGO FIESTA 2018 – VIBE KAMA LOTE YAACHA GUMZO MOROGORO

Msanii wa Bongo Flava - Ben Pol akitumbuiza katika ufunguzi wa matamasha ya mwaka huu ya Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana usiku. Tamasha hilo linahamia katika mji wa Sumbawanga mwisho wa wiki hii. 
Msanii wa Bongo Flava - Dogo Janja  akitumbuiza katika ufunguzi wa matamasha ya mwaka huu ya Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana usiku. Tamasha hilo linahamia katika mji wa Sumbawanga mwisho wa wiki hii. 
Msanii wa Bongo Flava - Nandy akitumbuiza katika ufunguzi wa matamasha ya mwaka huu ya Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana usiku. Tamasha hilo linahamia katika mji wa Sumbawanga mwisho wa wiki hii. 

Wasanii wa Bongo Flava - Roma (kushoto) na Stamina (kulia) wanaounda kundi la Rostam wakitumbuiza katika ufunguzi wa matamasha ya mwaka huu ya Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana usiku. Tamasha hilo linahamia katika mji wa Sumbawanga mwisho wa wiki hii.

Wasanii wa nyumbani wafanya makubwa kuwapagawisha mashabiki huku tamasha likihamia Sumbawanga

 Msimu wa Tigo Fiesta 2018- Vibe Kama Lote, umeanza kwa kishindo katika viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro huku wasanii wa nyumbani wakifanya onesho bab-kubwa lililoacha gumzo midomoni mwa maelfu ya mashabiki waliofurika kushuhudia tamasha hilo la kila mwaka.

Milango ilifunguliwa saa kumi na mbili kamili na kushuhudia wasanii wanaochipuka walioshiriki katika shindano la kusaka vipaji la Tigo Fiesta 2018 – Supa Nyota wakifungua jukwaa. Wasanii hao wachanga kutoka mjini Morogoro waliongozwa na washindi Supa Nyota kimkoa, Michael Yusufu (Belly 255) na Abdul Michael (V Dax).

Shangwe kubwa zaidi zililipuka wakati kundi linalokuja kwa kasi la Mesen Selekta pamoja na msanii Whozu anayetambaa na wimbo wake wa Huendi Mbinguni walipopanda jukwaani na kusababisha vumbi kutifuka miongoni mwa mashabiki huku wengi wakisikika wakinongona kuwa vijana hao ni moto wa kuotea mbali katika tasnia ya sasa ya bongo flava.

Wasanii wengine waliofanya kazi kubwa kukonga mioyo ya mashabiki ni pamoja na kundi la Rostam linaloundwa na wasanii Roma na Stamina, , Fid-Q aliyeambatana na msanii wa kike wa mziki wa kufokafoka Rosaree, Ben Pol, Mr Blue Kabayser, Dogo Janja, Maua Sama , Nandy, pamoja na Belle 9 ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kupanda jukwaani kama msanii mwenyeji wa Morogoro. Wasanii wote walionesha uwezo mkubwa wa kuimba na kumiliki jukwaa, huku wote wakiwa wamejiandaa kikamilifu pamoja na wacheza dansi waliokuwa wamevalia sare za kuvutia. 

Msanii mkongwe ambaye pia ni Mbunge wa Mikumi – Professor Jay ambaye aliambatana na wasanii wengine wakongwe ikiwemo Black Rhino waliwashangaza mashabiki ambao hawakutegemea ujio wa wasanii hao wakongwe kwa kufanya onesho la kukata na shoka, na kuwafanya hata wale waliokuwa wameanza kutoka uwanjani kurudi ndani na kukesha hadi jogoo wanawika.

Akizungumza katika onesho hilo lililoshirika 100% wasanii wa nyumbani, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe alisema kuwa mbali na shamrashamra za mwanzo wa msimu wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote, msimu huo ulikuwa umeibua fursa nyingi za biashara katika mji huo.

‘Tunatambua mchango mkubwa wa kiuchumi na kijamii unaotokana na tamasha la Tigo Fiesta. Bali na kutoa fursa ya kuutangaza mkoa wetu, pia imeongeza idadi ya wageni na kusababisha ongezeko kubwa la fursa za biashara kwa wamiliki wa hoteli, migahawa, mama nitilie, vyombo vya usafiri kama vile bodaboda, kumbi za starehe na biashara nyinginezo,’ alisema mkuu huyo wa mkoa.  

Kuendana na msimu wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote, kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali ya Tigo pia inaendesha promosheni za kusizimua kwa wateja wake ikiwemo ile ya kutoa punguzo kubwa la bei kwa tiketi zitakazonunuliwa kupitia Tigo Pesa Masterpass QR. Wateja wanapaswa kupiga *150*01#  na kuchagua 5 (lipia huduma) kisha kuchagua namba 2 (lipa Masterpass QR) na kutuma kiasi husika cha tiketi kilichotangazwa kwa kila mkoa husika kwenda namba ya Tigo Fiesta 78888888.

Wateja wa Tigo pia wanapata faida zaidi kupitia shindano la Tigo Fiesta 2018 – Chemsha Bongo Trivia linalotoa zawadi za kila siku za TSH 100,000, zawadi za kila wiki za TSH 1 milioni, simu janja za mkononi za thamani ya TSH 500,000 kila moja, pamoja na donge nono la TSH 10 milioni. Kushiriki wateja wanapaswa kujiunga kwa kutuma neno MUZIKI kwenda 15571 au kutembelea tovuti ya  http://tigofiesta.co.tz na kuchagua Trivia.

Huu ni mwaka wa 17 wa tamasha la muziki na kitamaduni la Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote ambapo mwaka huu litashirikisha 100% wasanii wa nyumbani watakaozuru mikoa 15 ya nchi ikiwemo; Morogoro, Sumbawanga, Iringa, Singida, Songea, Mtwara, Moshi, Tanga, Muleba, Kahama, Mwanza, Musoma, Arusha na Dodoma, huku kilele kikifanyika Dar es Salaam

No comments: