Askari wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Kisiwani Pemba, wakiwa katika zoezi la kutoa miili ya marehemu waliopoteza maisha katika ajali ya kuangukiwa na ukuta wa tanki la maji eneo la Machomanne Chake Chake Pemba leo.
Wananchi wakiuangalia mnara wa tangi la maji ulioanguka na kupoteza maisha ya wananchi watatu leo asubuhi.
Wananchi wakiuangalia mnara wa tangi la maji ulioanguka na kupoteza maisha ya wananchi watatu leo asubuhi.
Daktari bingwa kutoka Cuba anayefanya kazi zake Kisiwani Pemba, (jina halikufahamika) akimtibu mmoja kati ya majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Chake Chake baada ya ajali hiyo.
JUMLA
ya watu watatu wamefariki dunia papo hapo na watatu kujeruhiwa baada ya
kuangukiwa na ukuta wa mnara wa tanki la maji uliopo Machomanne Chake Chake
Pemba, leo saa tatu asubuhi.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Suleiman
Hassan Suleiman, amesema kuwa, merehemu hao walifikwa na mauti wakiwa katika
kazi ya kuteremsha ukuta wa mnara wa tanki la maji ambao walikuwa wameshaukata.
Kamanda alisema
kuwa idadi ya mafundi waliokuwepo kazini hapo walikuwa ni 12 ambapo watatu
wamepoteza maisha papo hapo na watatu kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya
Chake Chake na wengine sita walikimbia na jeshi la polisi liko katika utaratibu
wa kuwatafuta kwa ajili ya kuelewa hali zao.
Kamanda Suleiman
aliwataja marehemu hao kuwa ni Juma Rashid Juma (35) mkazi wa Chanjaani,
Suleiman Mohammed Abdiadi 'maarufu kama Golo' (55) mkazi wa Kwale na Salum
Muhidini Vuai 'Bandudu' (35) mkazi wa Madungu wote wakazi wa wilaya ya Chake
Chake mkoa wa Kusini Pemba.
Na majeruhi
katika ajali hiyo ni pamoja na Jackson John (26) mzaliwa wa Iringa na mkazi wa
Msingini, Ali Saleh Ali (35) mkazi wa Michakaeni na Yohana Richard (25) mkazi
wa Machomanne Chake Chake Pemba.
No comments:
Post a Comment