Friday, July 5, 2013
WAPELELEZI KUTOKA CHINA WAIBUA MAPYA KUHUSU MILIPUKO YA BOMU JIJINI ARUSHA…..WASEMA WALIPUAJI NI WAKAZI WA ARUSHA WENYEWE..!!
TAARIFA za awali kutoka kwa makachero wa Jeshi la Polisi nchini zimefanikiwa kubaini mtandao wa ulipuaji mabomu katika jiji la Arusha, imefahamika. Mpaka sasa taarifa zinadai mtandao uliohusika na milipuko miwili iliyotokea kwa nyakati tofauti jijini hapa ulipangwa ndani ya jiji la Arusha.
Mlipuko wa kwanza ulitokea katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu, wakati mlipuko wa pili ulitokea Uwanja wa Soweto Juni 15, mwaka huu na kuua watu wanne, huku majeruhi wa matukio yote wakifikia zaidi ya 100.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) jana jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema mbinu hizo zimejulikana kutokana na wananchi waliojitokeza kuwasilisha ushahidi kwa vyombo vya dola.
Alisema mpaka sasa ushahidi unaonyesha kuwa mtandao wa waliolipua wa mabomu hayo ulianzia jijini Arusha, na kikubwa kabisa wanawashukuru wakazi wa Arusha waliokuwa wakifika kutoa ushahidi wa wahusika.
Akiwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliendelea kubainisha kuwa upelelezi wa matuko hayo mawili unaendelea kwa umakini mkubwa na kikubwa kinachoangaliwa ni kuepuka kukamata watu wasiohusika.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa aliwataka pia wanasiasa nchini kutoigeuza milipuko ya mabomu hayo kama njia ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Mulongo katika hotuba yake aliendelea kuwataka wanasiasa kuacha dharau na kueneza maneno yasiyo na ukweli juu ya Serikali, badala yake aliwataka kuheshimu taratibu za nchi ili vyombo vya dola visilazimike kutumia nguvu kukabiliana na watu au kikundi kitakachovunja sheria zilizowekwa.
Bomu hilo lilirushwa katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA), wakati kikihitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne jijini Arusha Juni 15, mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chama chake kinao ushahidi wa picha na sauti unaothibitisha kwamba polisi ndio wahusika wa mlipuko huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment