ALIYEKUWA Mlinzi mkuu (bodyguard) wa Rais wa Rwanda, Paul
Kagame, Luteni Joel Mutabazi, ametekwa na kikosi cha Jeshi la Uganda na
kukabidhiwa kwa Serikali ya Rwanda.
Taarifa za
kiintelijensia zinasema kuwa Luteni Mutabazi, alikuwa
akiishi nchini Uganda kwa hati maalumu ya ukimbizi ya Umoja
wa Mataifa, baada ya kutoroka nchini Rwanda pamoja na aliyekuwa Mkuu wa
Majeshi ya nchi hiyo, Faustin Kayumba Nyamwasa.
Luteni Mutabazi alitorokea nchini Uganda Oktoba 2011, baada
ya kutoroka jela yenye ulinzi mkali wa kijeshi ya Kami nje kidogo mwa
mji wa Kigali akituhumiwa kwa kuhusishwa na kutoroka kwa mkuu huyo wa
majeshi na kukimbilia Afrika Kusini. Alikuwa mlinzi mkuu wa Rais Kagame
mpaka mwaka 2010, alipotoroka na kukimbilia Uganda.
Mlinzi huyo pia anashutumiwa na Serikali ya Rwanda kwa kutoa
siri kwa Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa chini ya Majeshi ya
Umoja ya Kulinda Amani nchini Kongo, (MONUSCO) na kuwezesha kuchakazwa na
kushindwa kwa kikosi cha waasi wa M23.
Kutokana na tukio hilo, hivi sasa Serikali ya Rais Yoweri
Museveni,
imelazimika kumsimamisha kazi Mkuu wa Intelijensia wa Jeshi
la Polisi,Joel Aguma, ambaye alihusika kumteka na kumkabidhi Luteni
Mutabazi kwa Serikali ya Rwanda.
Hatua hiyo ya Aguma ilitafsiriwa kuwa ni mkakati wa kutii
amri ya
Serikali ya Rwanda, ambayo ilitoa hati ya kimataifa ya
kukamatwa kwa mlinzi huyo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Rwanda imekiri kumkamata
Luteni Mutabazi na kuzuiliwa katika jela maalumu ya kijeshi ya nchi
hiyo mjini Kigali.
Msemaji wa Polisi wa Rwanda, Damas Gatare alisema kuwa huo
ni mpango endelevu wa Serikali za Rwanda na Uganda wa kukabiliana na
maasi na majasusi kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwa sheria
itachukua mkondo wake.
Serikali ya Rwanda imesema kuwa Luteni Mutabazi,
atashitakiwa kwa kosa la ujasusi na uhaini na hakuna mtu yeyote nchini humo ambaye
atafanikiwa kuukimbia mkono wa sheria ambapo jeshi la nchi hiyo
linaendelea kuwasaka watu hao.
Hata hivyo, Mkuu wa Polisi nchini Uganda aliyesimamishwa
kazi anadaiwa kuhusika katika utekaji huo wa kumrudisha Rwanda, Luteni
Mutabazi, Oktoba mwaka huu, baada ya kuhudhuria kozi ya mwaka mmoja ya
makamanda iliyofanyika katika kituo cha Polisi cha Rwanda, ambapo
aliibuka mwanafunzi bora katika kozi hiyo.
Mlinzi huyo alitekwa Agosti 20, mwaka huu, saa 11 jioni
kutoka hotelini kwake alipokuwa katika harakati za kutaka kutumia mtandao wa
Skype,ambapo alikuwa anataka kutoka chumbani kwake na kwenda
sebuleni ili aweze kupata wireless intaneti.
Akiwa katika harakati hizo, ghafla walivamia makomandoo
watano wa Jeshi la Rwanda wakiwa na bunduki za AK 47.
Tukio la kuvamia makomandoo hao lilizua taharuki ambapo
Luteni Mutabazi, aliweza kupambana nao hali iliyowafanya makomandoo hao
kushindwa kumtia nguvuni.
Makomandoo hao wa Rwanda walipoona wameshindwa kwa kupata
kipigo,waliweza kutoa ishara ya kuomba msaada kwa wenzao wa nje
waliokuwa katika gari.
Baada ya kuongezeka kwa nguvu kwa makomandoo hao,
walifanikiwa kumvamia na kumfunika kwa nguvu kwa kitambaa kilichokuwa kimepakwa
dawa hali iliyosababisha kupoteza fahamu kwa mlinzi huyo wa zamani wa
Rais Kagame.
Habari za kiitelijensia kutoka nchini Uganda zinasema kuwa
Luteni
Mutabazi alichukuliwa kwa gari maalumu lenye namba za
usajili UAK 551B na kukimbizwa hadi mpakani mwa nchi ya Rwanda ambapo
alikabidhiwa kwa majeshi la Serikali ya nchi hiyo.
-Mtanzania
No comments:
Post a Comment