Kwa ufupi
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiko katika harakati za kupinga
uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, uliompa ushindi
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe.
Zitto
ambaye pia ni Mbuinge wa Kigoma Kaskazini, juzi aliibuka mshindi katika
maombi yake ya kuizuia Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumjadili na au
kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake, hadi kesi ya msingi kuhusu
suala hilo itakapokuwa imesikilizwa.
Kadhalika, chama hicho
kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, John Mnyika
kimesema kinaendelea na utekelezaji wa uamuzi wa Kamati Kuu wa kutompa
Zitto ushirikiano wa aina yoyote.
Wakili wa Chadema, Peter
Kibatala, alisema jana kuwa japo wanauheshimu uamuzi wa Mahakama,
hawajaridhika nao na kwamba wanakusudia kwenda Mahakama ya Rufani
kuupinga.
“Ingawa uamuzi huu ni Interlocutory (uamuzi usiomaliza
kesi), lakini sisi hatukuridhika nao. Hatukuridhika na uamuzi wa
kutupilia pingamizi letu la awali, hati ya kiapo na hata amri yenyewe ya
zuio la muda,” alisema Wakili Kibatala na kuongeza:
“Kuna namna
nyingi za kufanya kupinga uamuzi huo, kama vile kukata rufaa, kuomba
marejeo au namna nyinginezo. Kwa hiyo kwa sasa tunaangalia namna bora ya
kwenda Mahakama ya Rufani bila kuathiri matakwa ya kisheria.”
Wakili
Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), alisema kuna haja ya kuiomba Mahakama ya Rufani
kuuchunguza uamuzi huo kwa kuwa una athari si kwa Chadema tu, bali hata
vyama vingine dhidi ya wanachama wake.
Kauli ya Mnyika
Kauli ya Mnyika
Mnyika
kwa upande wake alisema kutompa ushirikiano Zitto ni uamuzi wa Kamati
Kuu ambao ulitokana na hatua yake ya kwenda mahakamani kwa masuala ya
chama, kinyume cha matakwa ya Katiba ya Chadema na Kanuni zake.
Mnyika
alikuwa akirejea taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa, baada ya kikao hicho akiwataka viongozi wa ngazi zote za
chama hicho, wanachama, mashabiki na wapenzi wake, kutoshiriki wala
kusaidia kwa namna yoyote mikutano yote ya nje, ndani au shughuli
nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto na mawakala wake.
Ushindi wa Zitto
Ushindi wa Zitto
Katika
maombi hayo namba 1 ya 2014, Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando,
Zitto aliiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda kwa CC ya Chadema, hadi
kesi yake ya msingi namba 1 ya 2014 aliyoifungua mahakamani hapo
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Awali, mawakili wa Chadema,
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Kibatala walipinga
maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika
uamuzi wake juzi, Jaji John Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili
Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
Maombi
hayo ya Zitto yaliyotolewa uamuzi juzi yalitokana na kesi ya msingi
aliyofungua mahakamani hapo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini
wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema.
Katika kesi hiyo anaiomba
mahakama ikizuie chama hicho, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi
kumchukulia hatua zozote au kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi
hapo rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama hicho kupinga
kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia aliiomba Mahakama Kuu
imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za CC za
kumvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie
walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge
wa Kigoma Kaskazini. Kesi hiyo ya msingi imepangwa kutajwa mahakamani
hapo Februari 13, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment