MAAZIMIO YA
KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA
NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU HATUA ZA KINIDHAMU DHIDI YA WANACHAMA
ZITTO ZUBERI KABWE, DR. KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA
UTANGULIZI
Kamati Kuu ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao
cha dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka
ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama yaliyokuwa
yanawakabili
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa
Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa
Arusha Samson Mwigamba.
Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar es
Salaam
kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati
Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi
ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Aidha,
Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda
ya kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili
na kuamua suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri
hiyo ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka
dhidi yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote
watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu
ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za
Uendeshaji
Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya
Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi
za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana
na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama
ifuatavyo:
- Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
- Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;
- Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao halali vya Chama;
- Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;
- Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
- Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama;
- Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
- Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
- Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;
- Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
- Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.
UTETEZI WA
WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote
walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa
maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito wa
Kamati
Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele yake. Hata hivyo, siku ya utetezi wao,
ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na
kujitetea
kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki
katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr.
Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba – alikanusha
na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na
Mwongozo
wa Chama.
Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma
mojamoja na kwa ujumla wake dhidi ya[ke]”, na kwamba mashtaka hayo
sio ya kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha, licha ya
kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba
mwaka jana kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu
anayejulikana kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu
kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa wala
kushirikisha … wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi
na Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya
Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii
aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari
kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA
ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO
Itakumbukwa
kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo
na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi
Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko. Aidha, Zitto Zuberi
Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo
kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi
na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi. Hata hivyo, wakati
wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba
yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing
juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia
umethibitishwa
na mawasiliano ya baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe
kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu
mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua
madaraka.
Zaidi ya hayo,
baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko
ya Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama
wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko
ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa
kushirikisha
ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata kujadili suala
hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao kwa Msajili
wa Vyama vya Siasa.
Kuhusu tuhuma
zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama
unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha
Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi
hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha
zilizowasilishwa
mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na Zitto
Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo
alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee
Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi zilivyopokelewa na
kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu
walivyohudhuria
yeye na Zitto Zuberi Kabwe.
Zaidi ya hayo,
Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa
vya Chama kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo
uamuzi wa manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe
ni wajumbe na walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo
alionyeshwa
ushahidi wa maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna
yoyote ile katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha
saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo. Aidha, Dr. Mkumbo
hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote
na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile Kamati
Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto
Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa
hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya,
Dr. Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI YA
KAMATI KUU
Baada ya
kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji
kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati
wa Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe
kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo
ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa
wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo
za ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa
ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa
na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.
Kamati Kuu
imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa
na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia
vitambulisho
bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa
kukibomoa
Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu. Mkakati huo ulihusisha
pia hujuma dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi
mbali mbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma
Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja
kwa moja.
Kwa sababu zote
hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
- Kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na
- Kwamba, kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.
------------------------------ --
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment