Mara
baada ya kuwasili salama jana jioni katika hoteli ya Sueno Beach Side
eneo la Manavgat pembezoni kidogo ya jiji la Antalya nchini Uturuki, kikosi cha klabu bingwa nchini Tanzania bara Young
Africans leo asubuhi kimeanza mazoezi ya kujiandaa na mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu pamoja na mashindano ya kimataifa barani Afrika.
Yanga iliwasili huko majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za huko ikiwa
ni sawa na saa 12 kwa saa za Afrika Mashariki na moja kwa moja kikosi
kilielekea katika mji wa Manavgat ambapo ndipo ilipo hoteli ya Sueno
Beach Side ambapo msafara mzima umefikia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumiwa Rockersports na afisa habari wa klabu hiyo Baraka Kizuguto, amsema hoteli hiyo ya Sueno
Hotel Beach Side ni hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano, ambayo ina
jumla ya vyumba 760, mabwawa ya kuogelea,viwanja viwili vya mpira vya
mazoezi kimoja kikiwa na nyasi za kawaida na kingine nyasi za bandia.
Kocha
msaidizi wa Young Africans Charles Boniface Mkwasa amesema anashukuru
kikosi chake kimefika salama na wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri
kiafya na kifikra hivyo anatarajiwa mazoezi yatakayoanza leo yatasaidia
kuiweka timu katika hali nzuri na kuwa tayari kwa mashindano.
"Kazi
yangu kubwa ni kukiandaa kikosi kiwe katika hali nzuri ili pindi
tutakaporejea nchini timu iwe fiti na tayari kwa ajili ya mashindano,
kwa hali ilivyo nzuri na mazingira naamini timu itabadilika na kurejea
nchini ikiwa katika kiwango cha kizuri cha ushindani" alisema Mkwasa
Young
Africans inatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya
timu ya Ankara Sekerspor iliyopo Ligi Daraja la Kwanza nchini Uturuki.
Aidha
timu ya Sivasspor iliyopo Ligi Kuu nchini Uturuki inayonolewa na
mchezaji wa zamani Real Madrid na timu ya Taifa ya Brazil Roberto Carlos
pia imeweka kambi katika hoteli ya Sueno na leo asubuhi kabla ya Young
Africans kuanza mazoezi waliweza kupiga picha ya pamoja na gwiji huyo.
No comments:
Post a Comment