Timu za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni
mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
zinashuka tena viwanjani kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania pointi tatu.
Azam yenye pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo
Shooting katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mgambo
Shooting ipo katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL ikiwa na
pointi 19.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa
mechi kati ya Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga ipo
nyuma ya Azam kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47. Hata hivyo, timu
hiyo ina mchezo mmoja mkononi.
Tanzania Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David
Mwamaja hivi sasa ina pointi 22 ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za
mwisho katika ligi hiyo itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi
Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Ligi itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu)
kwa mechi kati ya Ashanti United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Jumapili (Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na mechi
kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine), Kagera Sugar na
Ruvu Shooting (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa
Manungu), JKT Ruvu na Rhino Rangers (Uwanja wa Azam Complex), Azam na Simba
(Uwanja wa Taifa) na Mgambo Shooting na Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).
No comments:
Post a Comment