Bodi
ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja klabu
ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria
ushirikina uwanjani.
Simba
ilifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa
faini ya sh. 500,000. Pia imepigwa faini nyingine ya sh. 500,000 kwa makocha
wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi
kwenye mechi hiyo.
Naye
mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa
kidole.
Mbeya
City imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani kwenye
mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za Yanga na Coastal
Union zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa
za maji uwanjani wakati timu hizo zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo
wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga
mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya
sh. 500,000 kwa kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.
Pia
mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa
la kupiga uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile atakosa
mechi tatu za ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki
wake kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.
Nayo
JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye
mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vilevile
wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya
marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa vile havina hewa ya kutosha.
Kwa
upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana na
makosa mbalimbali ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji
(sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).
Kocha
Msaidizi wa Polisi Morogoro, John Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili
kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili katika mechi dhidi ya Burkina Faso.
Kiongozi
wa Lipuli, Hamis Kiemba na wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na Green Paul
watapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya
kwenye mechi dhidi ya Kimondo.
No comments:
Post a Comment