KAMANDA WA POLISI IRINGA RAMADHAN MUNGI |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimefungua jalada dhidi ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani
Iringa, Hassan Mtenga kikimtuhumu kutishia kujeruhi na kuua kwa njia ya maneno.
Akizungumza na waandishi wa habari
mkoani iringa, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema Taifa, Benson
Kigaila alisema Mtenga amefunguliwa jalada namba IR/RB/2014 katika Kituo Kikuu
cha Polisi mjini Iringa.
“Leo (jana) tunakutana na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi tukitaka kupata majibu ya lini Mtenga
(Katibu wa CCM) atakamatwa, kuhojiwa na kisha kufikishwa mahakamani kwa kosa la
kutishia kujeruhi na kuua kwa njia ya maneno,” alisema na kuongeza:
“Kiongozi huyo ((anamtaja) alitoa
vitisho hivyo kwa Ofisa wetu Mwandamizi wa Vikosi vya Ulinzi wa chama, Hemed
Sabula na pia kiongozi huyo amekaririwa na vyombo vya habari akisema wanatuhumu
na kazi iliyobaki kwa vijana wao baada ya kusema mkuu wao (anamtaja) ni
kutekeleza tu.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Ramadhan Mungi alipotafutwa na NIPASHE ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na madai
hayo, alisema polisi inachunguza madai hayo na ikijiridhisha kwamba mlalamikiwa
ametenda kosa hilo watamkamata na kumfikisha mahakamani.
“Ni lazima kwanza tujiridhishe na
kufanya uchambuzi wa kina katika hilo linalo lalamikiwa na Chadema lakini
kimsingi vyama vyote vinatuhumiana na kutengeneza tetesi ambazo wanazisambaza.
Ila tukiona yana ukweli mtu yeyote anayelalamikiwa na kufunguliwa mashitaka
tutamkamata na kumpeleka mahakamani” alisema..
Kwa upande wake, Katibu wa CCM mkoani
hapa, Hassan Mtenga alisema Chadema wanatapatapa kutokana na hofu ya kuanguka
katika uchaguzi huo kwa vile walipotakiwa na polisi kupeleka ushahidi wa madai
hayo hawajafanya hivyo.
No comments:
Post a Comment