Kamishna wa Polisi Isaya Mngulu |
Na Karoli Vinsent
INSPEKTA Jenerali wa
Polisi (IGP), Ernest Mangu amesema kuwa, ongezeko la
wananchi kutokuheshimu sheria zilizopo limeongezeka katika miaka ya hivi
karibuni, tofauti na zamani kwani waendesha boda boda hivi sasa nao wamekuwa
wakishiriki vitendo hivi viovu pindi ajali inapotokea barabarani.
Akizungumza kwa niaba ya IGP,
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Isaya Mngulu,
katika uzinduzi wa taarifa ya haki za binadamu ya mwaka jana ilioandaliwa na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alisema watu wamekuwa
wakijichukulia sheria mkononi dhidi ya raia wenzao, jeshi la polisi, vituo vya
polisi na mali nyingine za umma.
Alisema, wananchi wamekuwa wakitoa
uhai wa raia wenzao kwa tuhuma za uhalifu, mbaya zaidi hata walinzi wa raia na
mali ambao ni jeshi la polisi, ambapo askari wake wamevamiwa na kuuawa, vituo
vya polisi vine mwaka jana vimevamiwa na wananchi pia mali za umma na binafsi
ziliharibiwa vibaya.
“Kwa kweli hali hii haiwezi
kuvumilika kuendelea kutokea katika nchi yetu. Nisihi jamii itambue umuhimu wa
kuheshimu utawala wa sheria na kuamini vyombo vya usimamizi wa sheria,” alisema
na kufafanua kuwa, kufanya vurugu na kushambulia raia wengine wakati vyombo
vilivyowekwa kisheria vipo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Pia alisema kuwa, haki ya kuishi ya
raia walio wengi imekatishwa na ajali ambazo mara nyingine zingeweza kuepukika
ingawa wahenga wanasema ajali haina kinga, ila barabara zikitumiwa vizuri ina
kinga.
Vile vile alisema kuwa, hivi sasa
taifa liko kwenye mchakato wa kutunga katiba mpya, hivyo ni vyema ikatumiwa
fursa hiyo ya kuandika katiba mpya kwa kuweka misingi madhubuti ya ulinzi wa
haki zote za binadamu hasa zile za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni pamoja na
zile za makundi maalum ambazo hazikulindwa na katiba ya sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji
wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba alisema kuwa, taarifa hiyo iliyozinduliwa ni ya
kumi na moja tangu kuanzishwa kwa uandishi wa taarifa ya aina hiyo mwaka 2002.
Alisema, taarifa hiyo inatoa maelezo
ya kina ya mambo mengi yahusuyo haki za binadamu na hali ya kusuasua katika
kuchukuliwa hatua stahiki lakini pia muelekeo wanchi katika kulinda na
kusimamia haki zote za msingi.
“Mfano tumetambua hatua
zilizochukuliwa baada ya operesheni tokomeza ambapo kuna mawaziri waliowajibika
na kuwajibishwa lakini tunapendekeza serikali isikomee hapo bali waliotekeleza
operesheni hizi nje ya utaratibu wachukuliwe hatua katika ubinafsi wao na
waathirika walipwe fidia za haki,” alisema.
Alimalizia kuwa, katika mchakato wa
kupata katiba mpya, wanawashawishi watanzania wote kuona umuhimu wa
kufuatilia mchakato hata kwa sasa ambapo unaonekana kutokwenda kama ilivyokuwa
imetarajiwa.
“Katiba
hii ni yetu na taifa hili ni letu tusipofuatilia ikija katiba mbovu waathirika
wa kwanza ni sisi na ikija nzuri wanufaika ni sisi,” alisema
No comments:
Post a Comment