Mkuu
wa Wilaya wa Songea Mjini Joseph Mkirikiti akikata utepe kuashiria ufunguzi wa
duka jipya la Tigo lililopo mjini Songea mtaa wa Shafi Bora asubuhi ya leo
mkoani Ruvuma. Wakishuhudia kutoka kushoto ni Meneja wa Mauzo wa Tigo wa mkoa
wa Ruvuma Kelvin Mibazi na Meneja wa duka hilo kutoka Tigo Wilfred Nestory.
Tigo leo imefungua duka jipya la huduma kwa wateja mjini
Songea ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma zake kwa wateja wa mjini hapo
ambao awali walikuwa hawana namna ya kupata huduma za moja kwa moja kutoka
kwenye kampuni hiyo ya simu.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mkuu wa
Wilaya wa Songea Mjini Bw. Joseph Mkirikiti, ambaye ameipongeza Tigo kwa hatua
yake ya kuzidi kusogeza karibu huduma zake kwa watu wa Songea.
“Pamoja na utatuzi wa kero za
mawasiliano naamini ya kwamba duka hili jipya litakuwa kama kituo cha kutoa
huduma mbali mbali ambazo wateja wenu wa Songea watakuwa wanahitaji kutoka
kwenu kila siku,” alisema Mkirikiti.
Bw. Mkirikiti alisema kwamba huduma
mbalimbali za mawasiliano zitolewazo na kampuni ya simu ya Tigo kama vile
kupiga simu, kutuma SMS, mtandao wa Intaneti pamoja na huduma ya kutuma na
kupokea fedha, zimekuwa kichocheo kikubwa katika kuleta maendeleo ya kijamii na
kiuchumi nchini. “Aidha huduma hizi zimeleta mageuzi chanya katika ufanyaji
biashara na kuinua hali ya maisha ya maelfu ya Wanasongea na mamilioni ya
watanzania kwa ujumla,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini Bw.
Jackson Kiswaga, amesema tawi hilo ambalo linalopatikana Songea mjini mtaa wa
Shafi Bora linatarajia kuwahudumia wateja wapatao 150 kwa siku kwa kuwapa
huduma mbali mbali za Tigo zikiwemo huduma ya kuunganishiwa intaneti, usajili
wa laini za simu, Tigo Pesa na huduma maalum za simu za kisasa (“Smartphones”).
“Duka hili lina manufaa makubwa kwa wateja kwa sababu
limeleta huduma zetu karibu zaidi kwao. Pia linapatikana sehemu nzuri
kibiashara kiasi kwamba litavutia hata wateja kutoka wilaya zingine na maeneo
jirani kama Mbinga, Namtumbo, Tunduru Songea vijijini na Nyasa,”alisema
Kiswaga.
Duka hili linatoa huduma nyingine maalum zikiwemo uuzaji wa
bidhaa mbali mbali kama simu za kisasa ambapo mteja anaruhusiwa kuzijaribisha
kabla ya kununua. “Hii inamuwezesha mteja kufanya uamuzi sahihi katika kuchagua
na kununua bidhaa inayokidhi mahitaji yake.”
Tawi la Songea linafikisha jumla ya maduka yanayoendeshwa na
kampuni ya Tigo nchini kufikia 40. Kwa mujibu wa Kiswaga, kampuni hiyo ina
mipango ya kufungua maduka mengine mengi zaidi katika sehemu mbali mbali
nchini.
|
No comments:
Post a Comment