SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wajumbe wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA) warudi bungeni akidai hawana sababu ya kwenda
kushitaki kwa wananchi kwa sababu watawacheka na kuwasikitikia, umoja
huo umemjibu wakisema wapo tayari kuchekwa.
Akihutubia vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi, siku moja kabla
ya sherehe za miaka 50 ya muungano, Rais Kikwete alisema kuwa huko nje
wanakotaka kwenda UKAWA siko na siku yake sio sasa, hivyo akawaomba
wasipoteze fursa hiyo muhimu ya kutoa mawazo yao bungeni ili yafanyiwe
kazi.
Alisema wananchi hawahusiki wala hawana namna ya kuwasaidia kwani mengi ya hayo yanayowakasirisha ni matatizo waliyoyazusha wao.
Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, aliliambia Tanzania Daima
Jumapili kuwa kama Kikwete anafikiri kwamba watarudi bungeni kwenye
mijadala ya dharau, ubaguzi na matusi inayofanywa na wajumbe wa CCM,
basi hajui chimbuko la tatizo.
“Kadiri anavyoendelea kuliacha Bunge liendelee na mijadala ya
kibaguzi na matusi, taifa linazidi kupasuka na washauri wake hawamwelezi
tatizo hilo,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atalitumbukiza
taifa kwenye machafuko ingawa yeye anafanya utani kwa kuipasua nchi na
kushangilia kauli za kibaguzi, kejeli na matusi zinazotolewa na baadhi
ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).
“Rais na wasaidizi wake inaelekea hawajasikiliza hata kauli
zinazotolewa na viongozi wa dini kuhusu rasimu ya Warioba, atuache
twende kwa wananchi, wao ndio wataamua.
Tumevumilia kwa kiwango fulani,
lakini itafika mahali uvumilivu utaisha, kwani hatuwezi kuendelea
kuzuiliwa kufanya mikutano na jeshi la polisi wakati mikutano ya Chama
Cha Mapinduzi(CCM) inafanyika kote nchini kutuchafua,” alisema Mbowe.
chanzo;TanzaniaDaima
No comments:
Post a Comment