Na Karoli Vinsent
WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Makame Mbarawa amewataka wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu nchini kuhakikisha wanatumia mitandao ya kijamii kwa maslahi ya taifa.
Kauli hiyo inatokana na matumizi mabaya ya mitandao kwa baadhi ya wanafunzi, walimu na watu mbalimbali, hali inayochangia kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa matukio ya uhalifu.
Rai hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam leo, wakati akizindua mradi wa mtandao wa Intaneti unaounganisha takribani vyuo vya elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti zipatazo 28.
Mbarawa alisema, mitandao ya kijamii inauwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya kimaendeleo hasa kupitia ushawishi waliokuwa nao wanafunzi na walimu katika kuibadilisha jamii kuwa na mtazamo chanya juu ya mitandao hiyo.
Alisema, miongoni mwa hasara zinazoweza kuwapata wanafunzi juu ya matumizi mabaya ya mitandao hiyo ni kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
“Naamini jamii itabadilika, kwani kuna sheria tatu ambazo zimetungwa ili kudhibiti matumizi mabaya kama Sheria ya matumizi ya Kompyuta, biashara na uhifadhi wa kumbukumbu katika kompyuta ambazo zote tunatarajia kuzipeleka Bungeni ili zipitishwe na kusimamia matumizi sahihi yenye tija kwa taifa” alisema Mbarawa.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuzungumzia mradi aliouzindua kuwa unalenga kuongeza idadi ya wahitimu wa vyuo vya juu wenye sifa stahiki katika maeneo ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Utawala kupitia mazingira ya kujifunza yaliyoboreshwa.
“Mradi huu umegharimu sh. bilion 4.6, ambao tulipendekeza kwenye maeneo manne kama Kukuza uchumi, kujenga uwezo wa Kuandaa Walimu watakaofundisha vyuo vikuu, kujenga uwezo wa taasisi maalum za elimu ya juu na uwekezaji wa TEKNOHAMA katika Sekta ya Elimu” alisema.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Mawasiliano inasimamia utekelezaji wa eneo la uwekezaji wa TEKNOHAMA inayounganisha Vyuo vya Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti ili kuongeza huduma za Maktaba kwa kutumia Elektroniki pamoja na Mfumo wa Kuhifadhi kumbukumbu za Elimu.
No comments:
Post a Comment