Katibu mkuu wa chama cha ACT TANZANIA--SAMSON MWIGAMBA akizungumza na waandishi wa habari ofisi za chama hicho kijitonyama jijini dar es salaam muda huu kuhusu mambo mbalimbali katika chama hicho |
Ikiwa imepita siku moja tangu umoja wa katiba ya
wananchi UKAWA kusaini makubaliano ya kuunganisha vyama vyao kwa lengo la kuwa
na nguvu zaidi ya kisiasa katika chaguzi zijazo nacho chama kipya katika siasa
za Tanzania cha ACT-TANZANIA kimeibuka
na kupongeza hatua hiyo na kuunga mkono harakati hizo za kisiasa za kuunganisha
nguvu ya upinzani kwa kusema kuwa kufanya hivyo itawasaidia kukiangusha chama
cha mapinduzi kirahisi huku akitoa tahadhari kwa muungano huo.
Akizungumza na wanahabari muda huu katika ofisi za
chama hicho kuhusu maadhimio ya mkutano wa kamati kuu ya chama hicho katibu
mkuu wa ACT Samson mwigamba pamoja na kutokuweka wazi kuwa chama chake kipo
tayari kujiunga na UKAWA amesema kuwa ni hatua nzuri kwa siasa za upinzani kama
muungano huo utakuwa ni muungano wa sera na kutetea wananchi huku akisema chama
chake kitaungana na chama ambacho kipo tayari kuwatetea wanachi na sio kwa
ajili ya kuiangusha CCM ili wagawane madaraka ya serikali.
“Muungano wa ukawa ni hatua nzuri katika siasa ila tunatoa tahadhari sana kwa muungano huo
usije ukawa ni muungano wa kugawana madaraka, sisi tutaungana na yeyote ambaye
yupo tayari kuwatetea wananchi ila hatutaungana na watu ambao watakuwa wanataka
kuiangusha CCM ili kuingia ikulu na kugawana madaraka”Amesema MWIGAMBA.
Aidha akizungumzia katiba iliyopendekezwa katibu mkuu
huyo amesisitiza kile ambacho na UKAWA walisisitiza kwa kusema kuwa katiba
iliyopendelezwa ni wizi na udanganyifu mkubwa kwa wananchi ambao umefanywa na
chama cha mapinduzi hivyo nao wanatangaza rasmi kuzunguka nchi nzima
kuwahamasisha wananchi wote kupiga kura ya hapana kwa katiba iliyopendekezwa
kwa kile walichodai kuwa haijakidhi mahitaji nya watanzania kwa sasa.
“Chama cha ACT kwa nia moja tumeamua kuzunguka kwa
watanzania wote kuhamasisha kura ya hapana kwa watanzania na zoezi hilo litaanza
mara moja kwa kuwa katiba hii iliyopendekezwa haijakidhi matarajio na maoni ya watanzania wote.
Akikizungumzia cha hicho kipya amesema kuwa ACT
kitazinduliwa rasmi tarehe 5 december mwaka huu jijini Dare s salaam ambapo kwa
mujibu wa katiba ya chama hicho kutafwatiwa na mkutano mkubwa wa hadhara wa
uzinduzi wa chama hicho ambao utafanyika jijini mwanza.
SOMA TAMKO LAO LOTE HAPA----
TAARIFA KWA UMMA
Maazimio ya Mkutano wa Tatu wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Tanzania
Uliofanyika Jumamosi Tarehe 25 Oktoba 2014 katika Hoteli ya Vina Jijini Dar es
Salaam
Kamati Kuu ya ACT-Tanzania ilifanya mkutano
wake wa tatu siku ya Jumamosi tarehe 25 Oktoba 2014 katika Hoteli ya Vina
Jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilijadili na kutoa
maazimio kuhusu hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kama
ifuatavyo:
1.
Kamati Kuu imejadili hitimisho
la mchakato wa Katiba Mpya katika ngazi ya Bunge Maalumu la Katiba. Kamati Kuu
imeendelea kusikitishwa na kushindikana kupatikana kwa maridhiano baina ya
makundi mbalimbali ya kisiasa nchini kuhusu mchakato na maudhui ya Katiba Mpya.
Kamati Kuu imesikitishwa zaidi na uamuzi wa Chama cha Mapinduzi na serikali
yake wa kuteka na kuburuza mchakato wa katiba kwa kuegemea matakwa ya sheria
bila kujali uhalali mpana wa kisiasa na kijamii nchini.
2.
Kamati Kuu imezingatia kuwa
mchakato wa katiba mpya umeitimishwa katika Bunge Maalumu la Katiba katika
mtindo ambao umeacha mgawanyika na mpasuko mkubwa wa kisiasa na kijamii nchini
badala ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa, ambalo ndilo lengo la msingi
la mchakato wenyewe.
3.
Kutokana maelezo ya hapo juu (1
& 2), bila kujali uzuri au ubaya wa maudhui yaliyomo katika Katiba
Inayopendekezwa, Chama cha ACT-Tanzania kitawashawishi wananchi kuikataa katiba
inayopendekezwa kwa kupiga KURA YA HAPANA katika kura ya maoni.
4.
Kamati Kuu imesikitishwa na
kuendelea kusuasua kwa kutolewa Ripoti kuhusu uchunguzi wa wizi wa fedha za
umma uliofanyika kupitia akaunti ya Escrow iliyotokana na mgogoro baina ya
TANESCO na IPTL. Kusuasua kutolewa kwa Ripoti ya Uchunguzu kumesababisha
kukwamisha bajeti ya serikali kwa kuwa wafadhili wamesimamisha misaada muhimu
kwa bajeti ya mwaka huu. Kamati Kuu inamtaka CAG atoe Ripoti yake kwa Kamati ya
PAC kwa ratiba iliyopangwa. Aidha Kamati Kuu inawaunga mkono wabunge wote walio
mbele katika kupigania sheria kuchukua mkondo wake katika sakata hili. Kwa
kipekee, Kamati Kuu imempongeza Mhe David Kafulila kwa ujasiri wake katika
kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa wote waliohusika na wizi wa
fedha za umma kupitia kivuli cha akaunti ya Escrow. Tunawahimiza wabunge
wazalendo wamuunge mkono mbunge mwenzao Mhe Kafulila katika kuhakikisha kwamba
uwajibikaji unapatikana katika kashfa hii kubwa kabisa kuikumba nchi yetu.
5.
Kamati Kuu imepokea taarifa ya
kuhusu ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo. Kamati Kuu
imesikitishwa na taarifa kwamba zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini hawatapata
mikopo. Kamati Kuu haikubaliani na hali hii na imewahimiza wanafunzi, vijana na
wadau wa elimu nchini kuungana na chama cha ACT-Tanzania katika kuishinikiza
serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanapatiwa mikopo ili
wawezi kujipatia elimu ya juu ambayo inahitajika sana kwa mustakabali wan chi
yetu.
6.
Uzinduzi rasmi wa chama
utafanyika katika jiji la Dar es salaam mnamo tarehe 05 Desemba mwaka huu. Kwa
mujibu wa katiba ya ACT TANZANIA kuna mkutano mkuu wa kidemokrasia (NATIONAL
DEMOCRATIC CONGRESS). Mkutano wa kwanza wa namna hiyo utafanyika Desemba 5. Tunatoa
wito kwa wanachama wote Tanzania kuanza maandalizi ya kushiriki mkutano huu.
7.
Kutakuwa na mapokezi makubwa na
mkutano mkubwa wa kwanza wa hadhara katika jiji la mwanza siku inayofuata
tarehe 06 dec 2014. Wito kwa wakazi wa jiji kufanya maandalizi makubwa
kukipokea chama mbadala
8.
Mwisho Kamati kuu imeazimia
kushiriki kwa nguvu zote uchaguzi serikali za mitaa na imeridhika na maandalizi
ya kupata wagombea katika ngazi ya mitaa,vijiji na vitongoji.
Samson Mwigamba
Katibu Mkuu
Jumatatu, 27 Oktoba 2014
No comments:
Post a Comment