Kundi lililoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
KUZALIWA KWA UKAWA
Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia
zoezi la uandikwaji wa Katiba Mpya, Tume ya kukusanya maoni chini ya
uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba ilifanya kazi yake vizuri na mwaka huu
katiba hiyo ilipelekwa Bungeni ambako Bunge Maalum la Katiba lilikutana
ili kupitia vifungu vyake kabla ya kuipeleka kwa wananchi kwa ajili ya
kuipigia kura ya kuikubali au kuikataa.
Kulitokea malumbano makali kati ya
wajumbe wa Bunge hilo juu ya vipengele kadhaa, hasa muundo wa serikali
ya Jamhuri ya Muungano. Wajumbe waliotokana na Chama Cha Mapinduzi,
walipendezwa na muundo wa serikali mbili kama ilivyo hivi sasa, wakati
wapinzani walitaka serikali tatu.
Misimamo hiyo ilileta utengano mkali
kiasi kwamba wajumbe wa upinzani wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba kuamua kususia vikao hivyo, wakipinga kile
walichokiita uchakachuaji wa rasimu ya katiba ya Jaji Warioba. Ususiaji
huo ulisababisha kuanzishwa kwa kundi lililoitwa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA).
Jaji Warioba
Kuanzishwa kwa umoja huo uliovihusisha
vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, kulisababisha kundi hilo
kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zijazo, wakianzia
na uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika katikati ya mwezi huu.
JAJI WARIOBA APIGWA
Baada ya wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba kumaliza kazi yake na kuikabidhi katiba pendekezwa kwa Rais
Jakaya Kikwete tayari kwa ajili ya kuipeleka kwa wananchi ili kupigiwa
kura ya maoni, kulikuwa na mkanganyiko miongoni mwa watu juu ya
kilichomo ndani ya katiba hiyo, baadhi wakipinga kuondolewa kwa vifungu
vingi vilivyokuwa na masilahi kwa nchi.
Miongoni mwa wanaoongoza harakati za
kupinga kuondolewa kwa baadhi ya vifungu vilivyowasilishwa na Tume hiyo,
ni Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo mara kadhaa imeandaa
mijadala ya wazi, lakini wakimtumia Jaji Warioba kama msemaji wake mkuu.
Kitendo hicho kimesababisha Warioba
kuonekana kama yupo katika mgogoro na chama chake na siku aliyofanyiwa
fujo na kupigwa katika ukumbi wa mikutano wa Ubungo Plaza, wanaodaiwa
kuwa makada wa CCM wanatajwa kuhusika.
Viungo vingi vya binadamu vikiwa vimetupwa katika machimbo ya kokoto yaliyopo Bunju, Dar.
VIUNGO VYA BINADAMU VYASHTUA
Jumatatu ya Julai 21, 2014, nchi
ilipatwa na mshtuko mkubwa baada ya kusambaa kwa habari kuwa viungo
vingi vya binadamu vilikutwa vikiwa vimetupwa katika machimbo ya kokoto
yaliyopo Bunju, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Watu wengi waliamini viungo hivyo
vimetokana na mauaji ya halaiki, hasa baada ya kukutwa kwa mabaki ya
mikono, miguu, mafuvu, viganja na vingine vingi. Lakini baadaye ikaja
kuthibitika kuwa viungo hivyo vilitupwa kimakosa na Chuo Kikuu cha
Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), ambacho pia kinaendesha
hospitali.
Viungo hivyo mbalimbali vya binadamu
vilikuwa vikitumiwa kimasomo na madaktari wanafunzi, ambavyo vilipaswa
kuteketezwa baada ya matumizi. Kitendo hicho kilisababisha serikali
kukisimamisha kwa muda chuo hicho kutokana na uzembe huo. Viungo hivyo
vya binadamu, hupatikana katika maiti mbalimbali zinazokosa ndugu wa
kuwazika na hutolewa na hospitali ya Taifa Muhimbili.
Aliyekuwa mshindi wa miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu kabla ya kuvuliwa taji.
Kitendo hicho pia kilikosolewa na
wachambuzi wa habari za kisiasa wakidai ulikuwa ni udhalilishwaji wa mtu
aliyewahi kuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo
kuhoji ulinzi wake.MISS
TANZANIA YAFUNGIWA MIAKA 2
Shindano la Miss Tanzania limejijengea
heshima kwa muda mrefu tokea lilipoanza tena mwaka 1994. Ingawa kumekuwa
na malalamiko ya chinichini juu ya kuwepo kwa hila, safari hii
lilijikuta likipata aibu kubwa, baada ya mshindi wake wa mwaka huu,
Sitti Mtemvu kudaiwa kudanganya umri hivyo kuibua sauti zilizotaka
kunyang’anywa kwa taji hilo.
Baada ya skendo hiyo kuchachamaa, Baraza
la Sanaa la Taifa liliendelea na uchunguzi wake dhidi ya malalamiko
mengi yaliyowahi kuripotiwa na katika tukio ambalo halikutarajiwa,
shindano hilo limesimamishwa kwa miaka miwili kutofanyika na sababu
nyingine iliyosababisha hatua hiyo, ni kugundulika kuwepo kwa rushwa ya
ngono katika hatua mbalimbali za shindano hilo linaloanzia vitongojini.