Wednesday, December 17, 2014

Wateja wa Tigo na ZANTEL sasa kufurahia huduma za kutuma na kupokea fedha kwa urahisi zaidi

Mkurugenzi wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha wa Tigo Andrew Hodgson akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo Zanzibar ya namna ya kutumiana fedha kati ya mteja wa TigoPesa na EzyPesa ambapo hakuna gharama za ziada anayoingia mteja anapotuma pesa kwa mtandao mwingine isipokuwa gharama zinakuwa sawa na zile zile anapotuma kwenye mtandao wake wa TigoPesa ama EzyPesa.  Kulia ni Meneja Chapa wa Tigo William Mpinga.
Mkurugenzi wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha wa ZANTEL Hashim Mukudi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano maalum ulioandaliwa kwa ajili ya kutangaza ushirikiano kati ya EzyPesa na TigoPesa mapema leo Zanzibar. Anayemfutia ni Meneja wa Biashara wa ZANTEL Zanzibar Mohamed Mussa, akifuatiwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha wa Tigo Andrew Hodgson na Meneja Chapa wa Tigo William Mpinga.

  1. Mkurugenzi wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha wa Tigo Andrew Hodgson (wa pili kulia) akipongezana na Mkurugenzi wa Huduma za Kutuma na Kupokea Fedha wa ZANTEL Hashim Mukudi mara baada ya kutangaza ushirikiano kati ya huduma zao za TigoPesa na EzyPesa mapema leo Zanzibar. Kutoka kushoto ni Meneja wa Biashara wa ZANTEL Zanzibar Mohamed Mussa, Meneja Miradi wa ZANTEL Shinuna Kassim na Meneja Chapa wa Tigo William Mpinga (kulia).
  1. Meneja Chapa wa Tigo William Mpinga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mjini Zanzibar mapema leo kuhusu ushirikiano kati ya TigoPesa na EzyPesa ambapo sasa wateja kutoka mitandao hiyo miwili wataweza kutuma na kupokea pesa kutoka mtandao hiyo moja kwa moja kutoka kwa wakala wa mtandao wao bila kuwa na ulazima tena wa mteja kutafuta wakala wa mtandao wa mtu aliyemtumia pesa.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wateja wa Tigo na ZANTEL sasa kufurahia huduma salama na uhakika ya kutumiana fedha kwenye Mitandao yao kwa 100%


Zanzibar - 17 Desemba, 2014. Kampuni za simu za mkononi za Tigo na ZANTEL zamezindua rasmi huduma za kutumiana pesa miongoni mwa wateja wake Tanzania.  Mbali na huduma hiyo ya kutumiana pesa miongoni mwa wateja wa mitandao hiyo, wateja wa EzyPesa na TigoPesa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa kwa marafiki na ndugu walio katika mitandao hiyo popote pale nchini.

Kutekelezwa kwa mpango huo kunazifanya Tigo na ZANTEL kuwa viongozi wa huduma kama hiyo Duniani.  Haya ni matokeo ya makubaliano yaliyotangazwa mwanzoni mwa mwaka huu na EzyPesa, TigoPesa na Airtel Money.  

Jinsi Huduma hiyo inavyofanya kazi:

Wateja wa Zantel:
Wateja wa Tigo:
1.      Piga *150*02#
1.      Piga *150*01#
2.      Chagua: Chaguo la 1 (Tuma Pesa)
2.      Chagua: Chaguo la 1 (Tuma Pesa)
3.      Chagua: Chaguo la 2 (Tuma TigoPesa)
3.      Chagua: Chaguo la 5 (Tuma EzyPesa)
3.1.   Ingiza Namba ya TigoPesa
3.1.   Ingiza Namba ya TigoPesa
3.2.   Ingiza Kiwango
3.2.   Ingiza Kiwango
3.3.   Ingiza Neno la Siri
3.3.   Ingiza Neno la Siri
3.4.   Subiri Uthibitisho wa Ujumbe Mfupi wa Maneno
3.4.   Subiri Uthibitisho wa Ujumbe Mfupi wa Maneno

Hakuna gharama za ziada mteja anapotuma pesa kwa mtandao mwingine isipokuwa gharama zinakuwa sawa na zile anapotuma kwenye mtandao wake.  Wateja wanaopokea pesa kutoka mtandao mwingine wanaweza kutoa pesa kwa wakala wa mtandao wao na hapatakuwa tena na ulazima wa mteja kutafuta wakala wa mtandao wa mtu aliyemtumia pesa.

Akizungumza kutoka Zanzibar, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Fedha wa Tigo, Andrew Hodgson alisema: “Tunafuraha kupanua wigo kwa wateja wetu kwa ubia na Zantel.  Hatua hii ni muhimu hasa kwa Zanzibar ambapo fursa ya kukua kwa huduma za fedha kwa mitandao ya simu bado ni kubwa.”
Anasema kama ilivyo kwa huduma nyingine za simu kama milio ya sauti na ujumbe mfupi wa maneno, kuna fursa kubwa ya kuimarisha huduma kwa wateja kwa kushirikiana badala ya kushindana baina ya wadau katika sekta ya mawasiliano kwa kupanua huduma za kutuma na kupokea fedha kwa kutumia mitandao Tanzania.
Anafafanua zaidi kuwa kwa kufanya kazi na wadau wengine, kunawawezesha kupanua wigo wa wateja na hivyo kwa pamoja kutoa huduma ambazo ni bora zaidi, salama, na za haraka kwa wateja wa pande zote.
“Ubia ambao tumeingia leo sio tu utaleta karibu kampuni zetu, bali muhimu zaidi ni ukaribu wa wateja wetu kwa kuwapatia huduma za fedha za kielektroniki bora zaidi ambazo hawakuweza kuzipata hapo awali,” alisema Hodgson. 
Mkurugenzi wa Biashara wa Zantel, Mohamed Mussa, anasema Zantel inaendelea kutimiza ahadi ya kuwarahisishia huduma za fedha wateja wake kwa kufanya kazi pamoja na Tigopesa.

“Kwa kufanya hivi tunapanua wigo kwa wateja wetu, huduma hii inawawezesha zaidi wateja kutuma na kupokea fedha kwa urahisi zaidi,” anasema.

Anafafanua zaidi kuwa kwa huduma hii itasaidia kuimarisha huduma za fedha kati ya visiwa vya Zanzibar na Tanzania Bara.

“Zantel iko katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa ushiriki wa wananchi wa Zanzibar katika sekta muhimu ya fedha unaimarika na kukua.  Tumehakikisha kuwa mtandao wa mawakala wetu na watoa huduma wengine wako tayari kuwahudumia wateja wetu,” anasema

No comments: