JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO
YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI
TANZANIA
03/01/2015.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Ndugu zangu wanahabari;
Napenda nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi wa taharuki iliyotokea jana
tarehe 02 Januari, 2015 katika jiji la Dar es Salaam ikiwahusisha baadhi ya
vijana wanaojikusanya kwenye vikundi na kujiita Panya road na pengine
kusababisha hofu kubwa kwa wananchi.
Chanzo cha taharuki hiyo, kulitokana na kuuawa kwa kijana mmoja ajulikanae
kwa jina la Mohamed Ayub na wananchi tarehe 01/01/2015 katika maeneo ya Tandale
kwa Mtogole kwa tuhuma za wizi wakati wa mkesha wa sikukuu ya mwaka mpya.
Tarehe 02/01/2015 majira ya saa tisa mchana yalifanyika mazishi ya kijana huyo
katika makaburi ya Kihatu Kagera Mikoroshini na taarifa zilizokuwa zimelifikia
Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam ni kwamba baada ya mazishi hayo vijana
wenzake na marehemu walijipanga kufanya fujo ili kulipiza kisasi cha mwenzao
kuuawa. Aidha, kabla vurugu hizo hazijafanyika na kwa vile Polisi walishaona
dalili ya vurugu hizo, tayari walifanikiwa kuzidhibiti.
Baada ya vurugu hizo kudhibitiwa na Polisi, vijana hao walitawanyika kwa
kukimbia katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kuzua taharuki
kubwa kwa wananchi kwamba huenda kila walipokimbilia wanampango wa kuwafanyia
fujo raia wema, jambo ambalo wasingeweza kulifanya kwa vile Polisi walikuwa
wameimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji.
Kufuatia hali hiyo na Jeshi la Polisi nchini likiwa linaendelea na msako
mkali wa kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na uhalifu huo, tunawaomba
wananchi watulie, wasiwe na hofu na waendelee na majukumu yao kama kawaida.
Mpaka sasa tunawashikilia watuhumiwa 36 kwa mahojiano na uchunguzi
utakapokamilika tutawafikisha mahakamani mara moja.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa vijana hao wananojihusisha na
vikundi hivyo kuacha tabia hiyo mara moja. Tumejipanga vizuri katika mikoa yote
kuhakikisha kwamba nchi inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea
muhali mtu yeyote ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na
kutia hofu wananchi.
Wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa kupitia namba ya
simu 0754 78 55 57, namba za makamanda
au katika kituo chochote cha Polisi.
Imetolewa na:-
Advera John
Bulimba - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment