Taarifa kwa vyombo vya habari.
CHADEMA inajivunia Mabaraza yake katika shughuli zake za kila siku
za ujenzi wa Chama. Kama mtakumbuka mwaka jana Oktoba tulifanya uchaguzi wa ndani
ya Chama na kupata viongozi wa baraza letu katika ngazi zote.
Toka tuingie madarakani tumefanya
mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuzindua caucas
za wazee katika Mikoa mbalimbali, kushiriki katika siku ya Wazee duniani na
utatuzi wa migogoro ndani ya Chama ambalo ndio jukumu kuu la baraza hili.
Ndugu waandishi wa habari itakumbukwa
kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Wazee tuna jukumu kubwa katika kuhakikisha uchaguzi
unakuwa huru na wa amani, ndio maana Baraza linaandaa kongamano lenye ujumbe wa
“Wazee na mustakabali wa Taifa letu tunapoelekea
uchaguzi mkuu.” Lengo ni kuwakumbusha wazee majukumu yao ya msingi yaani kusimamia
maadili na hasa ya uongozi.
Kwa muda mrefu, marais ambao
kimsingi ni wenyeviti wa CCM wamekuwa na tabia ya kuongea na wazee wa Dar es
salaam na kila mara wamekuwa ni wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hivyo CHADEMA imeamua kuvunja
mwiko huu kwa kuwa kina amini kuwa wazee wa Dar es salaam wapo walio wanachama
na wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Kwa kutambua umuhimu wa wazee
na changamoto zinazowakabili tumeona ni busara kuwa na kongamano hili litakaloeleza
wajibu wa wazee tunapoelekea uchaguzi mkuu.
Wote tunajua binadamu anapitia
hatua nne muhimu za maisha nazo ni utoto, ujana, utu uzima na uzee. Wazee wengi
hapa nchini wanakumbwa na matatizo mengi hususani ya kutotambuliwa na kutengwa na
jamii. Serikali imeshindwa kuongeza pension ama kuwapatia makao yenye hadhi.
Tumeshuhudia wazee wengi wakiuawa kikatili katika maeneo mengi.
Hitimisho.
Tunapoelekea uchaguzi mkuu,
wazee tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika zoezi zima
la kuandikisha na kupiga kura. Lakini pia kuwashawishi watoto,wake zetu, waume zetu,
wajukuu zetu kushiriki kikamilifu.
Tuna jukumu la kutatua migogoro,
kushawishi na kusimamia maadili, kubwa zaidi ni kuwa na uthubutu wa kukemea viongozi
wanaopata madaraka kwa njia ya rushwa na ufisadi.
Tunahitaji wazee watakaosimama
kidete na kupaza sauti zao kukemea maovu na watenda maovu. Tunasikitika sana kuona
wazee ambao wangepaswa kuwa na msimamo wa kukemea kama alivyofanya baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakishindwa na badala yake kuwa sehemu ya maovu
kwa kuwatetea
Mgeni rasmi katika
kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Julai, 2015,
atakuwa ni Katibu Mkuu wa Chama, Dk. Willibroad Slaa, ambapo litatangazwa moja
kwa moja kupitia Kituo cha Televisheni cha ITV.
Imetolewa
leo Ijumaa, 3 Julai, 2015 na;
Hashimu
Juma Issa
Mwenyekiti
wa Baraza la Wazee CHADEMA.
No comments:
Post a Comment