MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro (pichani) amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3, baada ya kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kilichokaa leo kwenye Makao Makuu ya Shirikisho hilo, chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde .
Muro amefungiwa baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF mbele ya Kamati ya hiyo, ambayo ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo, akahukumiwa kutengana na kutojihusisha na masuala ya soka kwa mwaka mmoja,.
wakati shitaka lingine ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC. Katika shitaka hilo, Jerry alidaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao na kutowapa nafasi watani wao wa jadi (Simba) kuingia kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa bao 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni. “Kamati ilisikiliza kwa makini taarifa zake alipokuwa anazungumza na vituo vya Redio na kugundua alikuwa sahihi, hivyo hapa hana hatia,”kimesema chanzo. Hata hivyo, Jerry Muro amehukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao na inadaiwa hakutoa taarifa ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
Badala yake, imeelezwa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alifika mapema leo kabla ya kikao kwa ajili ya kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro amekwenda kwao Kilimanjaro kusafisha makaburi ya wazee wake. Lakini Kamati ikaamua kuendelea na kikao kwa mujibu wa kanuni na hatimaye kuchukua hatua ilizochukua. Hata hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF - See more at:http://www.bongohotz.com/2016/07/kamati-ya-maadili-tff-yamfungia-jerry.html#sthash.o7L5va52.dpuf |
No comments:
Post a Comment