Tiganya Vincent, MAELEZO- Dar es salaam
Wasomi na Wanazuoni mbalimbali
wamepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu zamani Edward Lowassa kushikana
mikono na kusalimiana wakati wa Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya ndoa
ya Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa na Anna Mkapa.
Wanazuoni hao wametoa kauli
hiyo leo katika mahojiano maalum na Idara ya Habari iliyokuwa ikitaka
kupata maoni yao kuhusu kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao kwa
jamii.
Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa hatua hiyo imeonyesha kuwa huo ndio
Utanzania ulivyo wa kutofautiana bila kugombana.
Amesema kuwa kitendo hicho
kimewaonyesha wananchi kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuondoa
tofauti zilizopo kuliko kutumia njia nyingine kama vile maandamano na
mabavu katika kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya matatizo.
“Kukutana kwa viongozi hao na
kupeana mikono wakati wa kusalimiana kunakumbusha utamaduni wetu
uliojingekea toka siku nyingi wa kutatua matatizo yetu kwa mazungumzo
bila kugombana au kutumia mabavu,”alisema Profesa Mkumbo.
Kwa upande wa Profesa Joseph
Semboja amesema kuwa amefurahishwa sana na kitendo kilichoonyeshwa na
viongozi hao kwani kimeuonyesha ulimwengu kuwa Watanzania ni watu wenye
Amani na upendo.
Amesema kuwa hatua hiyo
imeonyesha kuwa Watanzania wanaweza kuwa na tofauti lakini wakaendelea
kuishi pamoja na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii kwa
ajili ya maendeleo yao na Taifa lao.
Profesa Semboja amewataka
wananchi kujifunza kutokana na kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao
ambao wameonyesha kuwa ni lazima wakae pamoja kwa ajili kushughulikia
mambo muhimu ya maendeleo ya wananchi badala kuendeleza tofauti ambazo
hazina manufaa kwa Watanzania.
Amesema kuwa ipo haja ya kwenda
zaidi ya hapo kwa kuweka utaratibu wa kukaa pamoja na kujadiliana ili
kutatua vyanzo vya migogoro kwa ajili ya mustakabali mzuri wa Taifa
hili.
Profesa amesema kuwa sio sahihi
kutumia mfumo wa jino kwa jino kwani utaratibu huo ndio unaoweza
kusababisha kukua zaidi kwa migogoro na wakati mwingine unasababisha
umaskini kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwani muda mwingi wananchi
hawana muda wa kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa sababu ya
migogoro.
Naye Profesa Samwel Wangwe
amesema kuwa hatua ya viongozi hao kukutana na kupeana mikonop ni ishara
kwa Watanzania kujifunza kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa katika
kuleta muafaka mgogoro wowote kuliko kutunishiana misuli.
Amesema kuwa mazungumzo yana
nguvu kubwa katika kultea upatanishi katika migogoro mbalimbali inatokea
katika jamii kuliko kutumia njia nyingine ambazo zinaweza kusababisha
vurugu na uharibifu wa mali za watu na upotevu wa maisha ya watu.
No comments:
Post a Comment