TAARIFA KWA UMMA
CHAMA
cha ACT Wazalendo kimeshtushwa na tuhuma, kashfa, porojo na matusi
mbalimbali yaliyotolewa jana na msemaji wa chama cha Mapinduzi(CCM),
Ndugu Christopher Ole Sendeka dhidi ya Kiongozi wa chama chetu, ndugu
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto.
Kutokana na hayo chama kina masuala yafuatayo ya kusema kwa wanachama wetu na umma wa Watanzania kwa ujumla:
•
Chama chetu kinakaribisha uchunguzi juu ya mali na madeni ya Kiongozi
wetu, ndugu Zitto. Tutafurahi uchunguzi huo ukihusisha akaunti zake za
benki pamoja na mfumo wa maisha yake binafsi (Life Style).
Tunavitaka
vyombo vya uchunguzi vianze kazi hiyo mara moja kwani tunaamini kuwa
Kama kuna Kiongozi ambaye Mali, Madeni, Maslahi na Akaunti zake viko
wazi basi ni ndugu Zitto.
Ikumbukwe
kuwa Katiba na Kanuni za chama chetu huwataka Viongozi wote wa chama
kuweka hadharani tamko la mali zao na madeni, ndugu Zitto alitekeleza
matakwa hayo ya kisheria, na mali pamoja na madeni yake yako hadharani
na mtandaoni. Tunatambua chama tawala kinaweweseka na tunataka
kiondokane na ugonjwa huo wa kuweweseka,badala yake wachukue hatua za
uchunguzi dhidi ya ndugu Zitto.
•
ACT Wazalendo tunayo taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
CAG. Kupitia taarifa husika CAG ametoa Hati safi Kwa Shirika la NSSF Kwa
hesabu za mwaka 2014/15. Hajaona ufisadi wowote ule.
Sijui
msemaji wa CCM anatumia taarifa ipi ya CAG kusema kuwa NSSF ilinunua
Ardhi Kwa bei ya Shilingi Milioni 800 aliyomhusisha nayo Kiongozi wetu.
Kwa
mujibu wa barua ya CAG Kwa Uongozi wa NSSF (Management letter), Shirika
hilo halijanunua ardhi yoyote Kigamboni, bali Shirika limeingia ubia wa
Ardhi Kwa Hisa (Land for Equity).
Hivyo
ni vizuri mbwatukaji huyo wa Chama tawala akaeleza kwa undani Ufisadi
anaousema juu ya manunuzi ya ardhi kwa kunukuu ripoti ya CAG kaitoa
ukurasa namba ngapi katika ripoti husika.
Labda chama chake kina taarifa nyengine ya CAG tofauti na iliyowasilishwa kwenye Kamati ya PAC.
Rais
Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa chama tawala, amemteua aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kuwa Balozi. Kauli za Msemaji wa chama tawala
alizozitoa jana zikiaminiwa zina maana kuwa Rais na Mwenyekiti wa chama
chake anateua mafisadi kuwa mabalozi. Ni vizuri nyie wanahabari muulize
juu ya hili jambo.
•
Ni wajibu wa Viongozi wa chama cha ACT Wazalendo kuupinga ujinga popote
pale ulipo, Kiongozi wa Chama chetu, ndugu Zitto, anatekeleza wajibu
huo kwa Uzalendo mkubwa kwa Taifa lake.
Chama
chetu kiko pamoja naye katika kupinga Ufisadi mkubwa wa ESCROW ambao
chama tawala kimeukalia kimya, ufisadi wa Mabilioni ya HATI FUNGANI na
hata sasa anapowapigania Waandishi wa Habari nchini katika Kampeni yake
ya kupinga MSWADA MBAYA wa Habari.
Tunajua kuwa kampeni hii ya kupinga Mswada mbaya wa Habari ndiyo ambayo imezua ubwatukaji huu wa msemaji wa chama tawala.
Ni
muhimu Serikali na chama tawala wajue kuwa chama chetu kitaupinga
mswada huo ambao utakwenda kuua tasnia ya habari nchini mpaka pale
utakaporekebishwa. Porojo, kashfa na matusi havitaturudisha nyuma,
tutaisimamia hoja hii mpaka mwisho.
•
Tunamtaka msemaji wa chama tawala aache porojo, kashfa, vijembe na
matusi. Ni muhimu ajikite katika kukishauri chama chake kutekeleza ahadi
zake kwa wananchi. Sasa ni mwaka mmoja tangu wachaguliwe, lakini hakuna
madawa hospitalini, hakuna mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, hakuna
ajira mpya, hakuna kupanda mishahara kwa watumishi wa umma, hakuna hata
jiwe la msingi la Kiwanda kipya lililowekwa tokea Serikali ya awamu ya
tano iapishwe, mzigo imepungua bandarini, magari makubwa ya mizigo
yameamuriwa yapaki tu kwa kuwa sekta ya Usafirishaji imeuliwa, na maisha
ya Watanzania yamezidi kuwa magumu.
Hayo
ndiyo mambo ya msingi ya Watanzania, chama chetu kitaendelea kuisimamia
serikali katika mambo hayo Bungeni kama anavyofanya mbunge na Kiongozi
wetu wa Chama.
Mwisho
kabisa, tunapenda kujua kama haya aliyoyasema Ole Sendeka ndiyo msimamo
rasmi wa Chama chake au ni maneno yake mwenyewe,maana kama ni msimamo
wa chama chake,tutakuwa na mengine ya kusema.
"Taifa Kwanza, Leo na Kesho"
Habibu Mchange
Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa
ACT Wazalendo
Oktoba 29, 2016
|
No comments:
Post a Comment