Friday, August 25, 2017

Meya Mwita acharuka, awatolea uvivu NSSF

MSTAHIKI Meya wa   Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amesema kuwa jiji linatarajia kulikabidhi jengo la Machinga Complex  Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya jamii (NSSF), ili iweze kuliendesha na kurejesha fedha zilizotolewa na mfuko huo kama mkopo kwa halmashauri ya jiji kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.

Mstahiki Meya wa jiji la Dar es salaam Mh. Isaya Mwita akiongea na waandishi wa habari kuhusu sakata la NSSF mapema leo ofisini kwake Karim Jee jijini Dar es salaam

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, Meya  Mwita amesema kuwa halmashauri iliingia mkataba na NSSF wa mkopo wa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo .

Ameongeza kuwa katika hatua za ujenzi huo, mkataba  ulifanyiwa nyongeza ya shilingi bilioni 2.14 na hivyo kufikia jumla ya mkopo wa shilingi bilioni 12.14 lakini hata hivyo makabidhiano ya jengo hilo yalipofanyika mwaka 2010 gharama za ujenzi zilifikia bilioni 12.7.

“ Kinachonishangaza na kuniogopesha ni kwamba , tumejulishwa kuwa deni hilo hivi sasa linakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni 40, kwakuwa tumejirizisha kwamba hatuna uhalali wa deni hilo, nasema hivi, jengo hili nitalikabidhi kwa NSSF, waliendeshe wao, na kurejesha fedha za mkopo ambazo walichukua” amesema Meya Mwita.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiendelea kuchua picha  na matukio mbalimbali katika  mkutano na Meya wa jiji la Dar es salaam Mh. Isaya Mwita na waandishi wa habari uliofanyika mapema leo jiji Dar es salaam

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa mkataba wa jengo hilo, lilipaswa kuwa na ghorofa tano upande mmoja , ghorofa sita upande mwingine sambamba na kuhudumia wafanyabiashara wadogo wa dogo 10, 000 lakini chakushangaza NSSF walifanya tofauti na mkataba huo.

Amesema wakati wanakabidhi jengo hilo lilikuwa na ghorofa nne lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 4,206 jambo ambalo imefanya jiji kushindwa kufikia malengo yake ya ulipaji wa deni hilo na utoaji huduma kwa walengwa.

Meya Mwita alifika mbali zaidi na kusema kuwa, halmashauri ya jiji haikuhusika na usimamizi wa fedha zilizokopwa na kufanya kushindwa kuthibitisha gharama zilizotumika.

“ Mkataba wetu uliitaka NSSF kutoa fedha kwa halmashauri ya jiji  kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, jambo ambalo halikufanyika, fedha zilizoongezeka kutoka bilioni 12.14 hadi kufikia bilioni 12.7 ziliongezwa bila kufikia makubaliano yoyote kati ya jiji na NSSF” alifafanua Meya Mwita.

Hata hivyo Meya Mwita alisema kwa muda mrefu jiji limekuwa likijaribu kutafuta muafaka na NSSF kuhusu namna ya ulipaji kodi jambo ambalo halikufanikiwa na kusisitiza kwamba , kamwe jiji halitalipa deni hilo kwakuwa haina uwezo wakulilipa.

                                    NA CHRISTINA MWAGALA, OFISI YA MEYA WA JIJI



No comments: