Thursday, February 1, 2018

MAHAKAMA KUU NCHINI KENYA YAINGILIA KATI SAKATA LA ODINGA

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru kuwashwa kwa vituo vya habari vitatu binafsi na serikali na kuiagiza serikali kutoingilia utendaji kazi wa vituo hivyo hadi kesi hiyo itakaposikilizwa kikamilifu.
Juzi, Jumanne matangazo ya vituo vya KTN, NTVna Citizen TV yalizimwa ghafla na serikali baada ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya kuzima mitambo yao kuepusha vituo hivyo kurusha moja kwa moja mkutano wa kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kama Rais wa watu wa Kenya ambapo bado haijulikani kama serikali wataifuatilia agizo hilo.

Sherehe ya kuapishwa kwa Raila ilichukuliwa na wengi kama mzaha lakini serikali imeshikilia kuwa kitendo hicho kilikuwa kinakiuka sheria za nchi hiyo na kwamba ni kosa la uhaini hivyo ilijaribu kuhakikisha taarifa hiyo haitawafikia Wakenya wengi ambao wangelifuatilia tukio hilo kupitia matangazo ya runinga.

Okiya Omtata, muwasilishaji mashtaka na mwanaharakati amesema anataka agizo la serikali litangazwe kuwa kinyume na katiba na vituo hivyo vifidiwe.
Wakenya wengi wamekosa matangazo ya runinga kwa siku tatu sasa. Vituo hivyo vilivyoathirika vimedai kupata hasara ya mamilioni ya dola za kimarekani.

Vituo hivyo vya binafsi vinategemea fedha za matangazo ya biashara na hawakuweza kupata fedha hizo kwa siku zote walizokuwa wamefungiwa ambapo Omtata ametaka serikali ilipie hasara za Citizen TV, KTN na NTV.
Kuibuka kwa mitandao ya jamii kumeathiri vyanzo vya mapato vya vituo vingi vya habari na kulazimika kuwafuta kazi mamia ya wafanyakazi wao ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Serikali ya Kenya ilitaka vituo hivyo vifungwe hadi polisi wamalize uchunguzi dhidi ya wanasiasa na waandishi walioshiriki katika sherehe ya kuapishwa kwa Bw. Odinga siku ya Jumanne.

No comments: