Wednesday, February 21, 2018

Naibu Waziri wa Afya afanya ziara Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza

Judith Ferdinand, BMG Habari
Naibu Waziri  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ametembelea hospitali ya Rufaa Kanda ya Ziwa Bugando iliyopo Jijini Mwanza ili kujionea namna shughuli mbalimbali za afya zinafanyika hospitalini hapo.
Dkt.Ndugulile alifanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo jana na kubainisha kwamba kati ya akina mama 100,000 wanaojifungua nchini, akina mama 556 hupoteza maisha na kwamba ili kupambana na changamoto hiyo, serikali imeweka mkakati wa kuboresha zaidi utoaji huduma za afya katika Vituo vya afya kote nchini.
“Kanda ya Ziwa ina vifo vingi vinavyotokana na kujifungua hivyo kuboresha vituo vya afya ni moja ya mikakati ya serikali katika kupunguza vifo hivyo kwa kujenga vyumba vya upasuaji, wodi ya akina mama na mtoto, maabara, kitengo cha dharura pamoja na kuweka gari la wagonjwa (Ambulance) litakalosaidia kumfikisha mgonjwa kupata huduma haraka”. Alisema Dkt.Ndugulile.
Alisema serikali inafahamu changamoto ya upungufu wa rasirimali watu katika  afya hivyo itaendelea kusomesha madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ambao watafanya kazi kwa kufuata maelekezo yake li wananchi wa maeneo husika wapate huduma bila kulalamika.
Pia alisema serikali itaendelea kuboresha huduma za afya mahospitalini ili kuweka mfumo vizuri wa rufaa kwa kila ngazi ya hospitali kufanya kazi kulingana na nafasi yake kama vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya, mkoa rufaa kanda na taifa.
Aidha alisema rufaa za wagonjwa nchini zimepungua kwani kwa sasa kuna taasisi zenye zinauwezo wa kutoa huduma ya matibabu ya magonjwa ya upasuaji mifupa na kansa ambayo ndio  magonjwa yaliyosababisha wagonjwa wengi kutibiwa nje ya nchi na kwamba hivi sasa kuna wagonjwa nje ya nchi ikiwemo Uganda hupata rufaa kutibiwa hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt.Abel Makubi alimshukuru Naibu Waziri Dkt.Ndungulile kwa kutembelea hospitali hiyo na kwamba aliyoshauri yatafanyiwa kazi.
Dkt.Makubi  aliishukuru wizara ya afya kwa kutoa shilingi milioni 420 kwa ajili ya dawa za kansa  ambazo hapo awali zilikua changamoto kwa wagonjwa wengi pamoja na kusaidia ujenzi wa jengo la kitengo cha kansa ambapo awamu ya kwanza imekamilika na inasubiriwa ujenzi wa awamu ya pili ya wodi.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndungulile (katikati) jana akiwa kwenye ziara ya kutembelea Hospitali ya Rufaa Bugando ili kujionea shughuli za utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo. Pia alitembelea jengo la kitengo cha Kanda na kuzungumza na Wakuu wa Idara mbalimbali katika hospitali hiyo. Wengine ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Bugando Dkt. Abel Makubi (kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi Huduma za Tiba katika hospitali ya Rufaa Bugando Dkt.Bahati Wajanga (kulia).




No comments: