Monday, February 19, 2018

NDUGU WA AKWELINE WAMEKUBALI KUUCHUKUA MWILI NA HAYA NDIO WALIYOYASEMA BAADA YA KUONA MWILI WA NDUGU YAO.

HATIMAYE ndugu wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyepigwa risasi Februari 16, 2018 wamekubali kuuchukua mwili wa ndugu yao huyo baada ya kususa kufuatia sintofahamu iliyoibuka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili walipoambiwa ripoti hiyo itatoka baada ya siku 14.Tokeo la picha la AKWELINE
Wakizungumza mara baada ya maafikiano baina yao na madaktari, wamesema wamepewa sehemu ya ripoti ya uchunguzi ambayo inaonyesha ndugu yao alifariki dunia baada ya kupigwa risasi kichwani hivyo wameridhika nayo na sasa wanakwenda kufanya kikao cha ndugu kujadili namna gani watampumzisha Akwilina.

Shemeji wa mwanafunzi Akwilina, Festo Kavishe amesema uchunguzi wa mwili huo, umeonyesha kwamba Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.

“Ripoti ambayo tumepewa imeonyesha kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa vibaya na risasi ambayo iliingilia upande wa kushoto kwa kichwa chake na kutokea upande wa kulia  ambao umefumuka vibaya,” amesema.

Kwa mujibu wa Kavishe, iwapo madaktari wasingewapatia majibu hayo wasingethubutu kuuchukua mwili huo kwa mazishi, kwa sababu walihitaji kupata picha kamili ya nini kilimuua Akwilina.

“Sasa tumeshafahamu nini hasa kimemuua ndugu yetu kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na madaktari baada ya uchunguzi, hivi sasa tunakwenda kujadiliana kuhusu mazishi yake,” amesema Kavishe.
Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.

No comments: