Wednesday, March 28, 2018

HIZI NDIYO SALAMU ZA SIKU KUU YA PASAKA KUTOKA KWA IGP SIRRO

Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro anawashukuru Wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Jeshi la Polisi  jambo ambalo limesaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa hapa nchini. 

Kiujumla hali ya usalama hapa nchini ni shwari na matukio  makubwa ya uhalifu wa kutumia Silaha yamepungua kwa kiasi kikubwa na jitihada za kukabiliana na makosa ya usalama barabarani zinaendelea ili  kupunguza ajali zinazosababisha vifo na majeruhi kwa raia.
Picha inayohusiana
Tunapoelekea kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi katika mikoa yote linawahakikishia wananchi kuwa limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sikukuu hii inasherekewa kwa amani na utulivu na hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyofanyika na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.

Ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi wote wanasherekea sikukuu hiyo katika hali ya  utulivu.

Wazazi wanatakiwa kuwaangalia watoto wao na kutowaacha kutembea peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa karibu, pia wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa  kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi hizo ikiwemo kutoruhusu disko toto na kujaza watu kupita kiasi.

Vilevile Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia Sheria za Usalama barabarani hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.

Nawatakia Pasaka njema.

No comments: