TAARIFA YA SAMSON MWIGAMBA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU WARAKA WA MKAKATI WA MABADILIKO 2013
Jana katika taarifa kwa waandishi wa habari, Mhe. Tundu Lissu na Mhe.
John Mnyika waliudanganya umma kuhusu waraka unaohusu Mkakati wa
Mabadiliko 2013. Katika maelezo yao waheshimiwa hawa, pamoja na mambo
mengine, walidai kuwa waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya
habari ni feki. Ukweli ni kwamba:
Ninathibitisha kwamba waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya
habari na mitandao ya kijamii ni sahihi neno kwa neno kama nilivyousoma
katika magazeti ya HabariLeo, Jamhuri na Rai, pamoja na nakala iliyopo
Jamii Forum. Ili kuthibitisha kwamba waraka ule ndio wenyewe,
nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta mpakato (laptop) yangu
ambako ndiko ulikoibwa na viongozi wa chama baada ya kunipora kwa nguvu
laptop yangu Oktoba 25 na kukaa nayo hadi jioni ya Oktoba 28.
Waraka huu si wa uhaini
wala mapinduzi wala usaliti kama inavyodaiwa na akina Lissu. Huu ni
waraka wa kusaka ushindi katika uchaguzi halali ndani ya chama ambao
ulikuwa ufanyike Desemba 2013, na ambao sasa umesogezwa mbele.
Napenda ijulikane
kwamba wakati wa uchaguzi si jambo la ajabu kuwa kwa wanachama kuwaunga
mkono wagombea tofauti. Nimekuwa karibu na Mwenyekiti Mbowe kwa miaka
mingi na ninajua kwamba yeye naye anao mkakati tena unaohusisha mbinu
haramu za kuhakikisha anammaliza Zitto na yeye kupita bila kupingwa
kwenye uchaguzi huo. Wanaoshiriki mkakati wake ni pamoja na Lema, Lissu
na wakurugenzi kadhaa waliopo makao makuu.
Waraka huu ulipaswa
kuwa siri ndani ya watu watatu tu (M1, M2 na M3) na haikutarajiwa kwamba
ungevuja kwa jamii. Bahati mbaya viongozi wa chama baada ya kuunasa
waraka huu kutoka kwenye komputa yangu mpakato (laptop), na baada ya
kikao cha Kamati Kuu, waliamua, kwa jazba na bila kutumia busara ya
kiuongozi, kuusambaza waraka huo kwenye vyombo vya habari kwa lengo la
kuwakomoa na kuwadhalilisha waandaji. Sasa baaada ya kugundua madhara ya
waraka huo machoni pa jamii wameamua kuukana. Ni ajabu kwamba wanaukana
waraka ambao waliusambaza wenyewe.
Nasisitiza kwamba mambo
yaliyopo kwenye waraka ni bayana na dhahiri. Sibahatishi kwa sababu
mimi nimefanya kazi makao makuu kama Mhasibu Mkuu hadi Mwezi Aprili
2012. Ni kwa kutambua uozo uliopo katika uongozi wa chama makao makuu
niliona umuhimu wa kubadilisha uongozi kwa njia za kidemokrasia ili
tukiokoe chama na hatukuwa na nia wala sababu za kuanika haya yote
kwenye umma. Kwa sababu za chuki na kukosa busara za kiuongozi huyo
anayeitwa Mwanasheria Mkuu akawashauri viongozi wetu kijinga wauanike
waraka mbele ya macho ya watanzania. Wangekuwa na akili na busara baada
ya yote haya kutokea wangejiuzulu au kuitisha uchaguzi mara moja.
Tunatambua kwamba
viongozi wetu wanamchukia Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa siku nyingi sana na
wametamani kumfukuza siku nyingi. Hata hivyo, ninawashauri watafute
sababu nzuri za kumfukuza uongozi na hata uanachama kwa sababu yeye
hahusiki na waraka wetu wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 hata chembe,
pamoja na kwamba yeye ndiye alikuwa na bado ndiye mlengwa mkuu, kama
atakubali.
Samson Mwigamba (M3)
Arusha
Jumatano, 27 Novemba 2013
No comments:
Post a Comment