Ripoti hizo zimedai kuwa waasisi
wawili wa chama cha Rwanda National Congress (RNC) akiwepo Dr.Theogene Rudasingwa
walikutana Dar Es Salaam pamoja na makamanda wa ngazi ya juu wa kikundi cha
waasi cha FDLR.
Ilidaiwa kuwa Mratibu wa chama cha RNC
Dr.Theogene Rudasingwa na mshauri wa chama hicho Condo Gervais walikiwakilisha
chama hicho cha upinzani huku kikundi cha waasi cha FDLR kikiwakilishwa na Katibu
mkuu Mtendaji Luteni Kanali Wilson Rategeka na Kanali Hamadi ambaye ni kamanda
wa operesheni
Gazeti hilo kupitia habari zake liliripoti
kuwa maofisa wa FDLR wanasafiri kwa kutumia hati za kusafiria (paspoti) za Tanzania.
Wiki moja kabla ya
ripoti hiyo, gazeti hilo hilo la Serikali ya Rwanda, liliandika habari kuwa Waziri
Mkuu wa zamani wa Rwanda Faustin Twagiramungu alikua nchini Tanzania tangu
Januari 19,2014 kabla ya kusafiri kuelekea jijini Lyon, Ufaransa ambako
alihudhuria mkutano wa wajumbe wa chama chake cha upinzani cha RDI (Rwanda
RWIZA).
Gazeti hilo lilimnukuu Twagiramungu akizungumza
mbele ya kikao hicho kuwa alikuwa nchini Tanzania kwa kile alichokiita ni
“Malengo Mahsusi”
Aidha gazeti hilo liliendelea kueleza
kuwa tarehe 20 Decemba, 2013 Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi
walisafiri kwa kutumia hati za kusafiria za Tanzania kuelekea nchini Msumbiji
kwa mazungumzo na watu wanaodaiwa kuwa ni mamluki wa chama cha RNC.
Ubalozi wa Tanzania Rwanda ulikanusha
tuhuma hizo kwa misingi ya kuwa idara ya uhamiaji ya Tanzania haina kumbukumbu
juu ya watu hao kuingia Tanzania na pia Rais Kikwete hakuwa nchini Tanzania
Tarehe 23/01/2014, hivyo madai kuwa alikutana na viongozi wa vyama hivyo au
kikundi cha waasi kwa nafasi yake, si kweli.
Pamoja na Serikali kupitia Ubalozi etu
nchini Rwanda kukanusha, kupitia taarifa hii kwa umma, tunaitaka serikali yetu
kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na;
1. Kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mtiririko wa tuhuma
hizo, hasa zile zinazohusu matumizi ya pasi za kusafiria ili kujiridhisha pasi
na shaka kuwa jina la nchi yetu halitumiki vibaya kuweza kuhatarisha uhusiano
wa kidiplomasia na majirani zetu tena ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
2. Kutokana na ukweli kuwa Idara ya Uhamijai ni moja ya
taasisi zenye uozo mkubwa unaoendana na vitendo vya rushwa, ni vyema serikali
ikajiridhisha na kuridhisha Watanzania kwa hakika kwamba hakuna maofisa wa juu wa serikali ya Tanzania kwa
maelekezo au sababu zao binafsi walishiriki katika utoaji wa hati za kusafiria
kwa watu hao wasiokuwa raia wa Tanzania katika hali inayotia shakani uhusiano
wetu na nchi jirani..
Matumizi mabaya ya hati ya kusafiria
kama utambulisho wetu kimataifa ni makosa makubwa yanayokiuka mikataba ya kidiplomasia,
sheria za kimataifa na yanayochafua sura ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa
endapo hati hizo zitaangukia mikononi mwa watu wabaya kama ilivyotokea miaka
miwili iliyopita pale ambapo utambulisho wa taifa letu (bendera) ulipotumika
katika meli za nchi moja kukwepa vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
3. Tunataka Bunge la Tanzania kupitia Kamati ya Mambo ya
Nje, kuunda kamati ndogo ambayo italifanyia kazi suala hili la uhusiano wa nchi
yetu na Rwanda ambao umekuwa ukionesha hali ya kulega lega kutokana na
chokochoko za maneno kutoka kila upande.
4. Aidha tunataka pia kujua msimamo wa Serikali ya
Tanzania juu ya kauli za Twagiramungu ambaye amenukuliwa akisema mbele ya kikao
cha chama chake kuwa alikuwa nchini kwa malengo mahsusi! Malengo hayo ni yapi?
Tangu taarifa hizo
zilipochapishwa, Serikali ya Rwanda imekaa kimya.Wizara ya mambo ya nje
haikuchukua hatua yoyote hata kumuhoji balozi wa Rwanda nchini Tanzania kutoa
msimamo wa serikali yake .Heshima ya Tanzania kimataifa imewekwa rehani kwa
tuhuma hizi nzito hasa kipindi hiki ambacho uhusiano wa Tanzania na Rwanda
ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki umeonekana ukilega lega
Mkataba wa Umoja wa Afrika
(AU Chartter) –Ibara ya 3(b) umeainisha kuwa kila nchi mwanachama zinatakiwa
kuheshimu uhuru na mipaka ya nchi nyingine bila kuingilia mambo ya ndani
isipokua pale ambapo Umoja wa Afrika unapoona haja ya kufanya hivyo kupititia
Kikao cha Mkutano mkuu wa Afrika au Ikiwa kuna janga kubwa linalohusisha mauaji
ya kimbari au uhalifu dhidi ya binadamu kwa mujibu wa Ibara ya 4(a), (b), (f)
ya kanuni za uendeshaji wa umoja wa Afrika,au nchi mwanachama inapoomba msaada
Sasa habari hizi kuwa Tanzania
inaingilia maswala ya ndani ya nchi nyingine ambayo ni mwanachama mwenza ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika ni hatarishi kwa mahusiano ya
kidiplomasia ambazo hazitakiwi kujibiwa kwa hoja nyepesi kuwa Rais hakuwepo
nchini muda huo bali tulitarajia serikali ingeenda mbali zaidi katika kufanya
uchunguzi wake na pia kuomba ufafanuzi wa misingi ya tuhuma hizo kutoka
serikali ya Rwanda kwa kuwa chombo kilichoripoti habari hiyo ni chombo cha
habari kinachomilikiwa na serikali ya Rwanda.
Hivi karibuni iliripotiwa
kuwa chama cha RDI kimetangaza kuwa kipo tayari kuuondoa utawala wa Kigali
madarakani kwa kutumia nguvu jambo ambalo ni kinyume na na ibara ya 4 ya mkataba wa uanzishwaji wa umoja
wa Afrika(AU) ambayo imekataza kutoitambua njia ya kubadili utawala kinyume na
taratibu za kikatiba na hivyo kuzuia serikali zilizoingia madarakani kwa njia
hiyo kushiriki shughuli za umoja huo.
Itakuwa ni jambo la fedheha
kwa nchi kama Tanzania kuingizwa katika mambo yanayozua mgogoro na hata kupelekea
kukwamisha malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata Umoja wa Afrika ambao
tulikubali kuhakikisha malengo ya utengamano kupitia taasisi hizi za kimataifa
yanatimia.
Kwa upande wa FDLR ikumbukwe kuwa
si chama cha siasa bali kikundi cha waasi ambacho Serikali ya Kigali imekuwa
ikikituhumu kwa kufanya mauaji ya kimbari (genocide) kule Rwanda. Ni fedheha
kwa serikali yetu kutochukulia kwa uzito suala hili linaloweza kutoa taswira
kuwa Tanzania ina ushirika na vikundi vinavyokumbatia itikadi inayopigwa vita
na jumuiya ya kimataifa.
Mbali na serikali kufanya
uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo, serikali ya Tanzania ilitakiwa kumuhoji
Balozi wa Rwanda juu ya msimamo wa serikali yake kutokana na habari iliyoandikwa
na chombo hicho ili kuboresha mahusiano mema kati ya Tanzania na Rwanda na pia
kwa maslahi mapana ya utengamano wa jumuiya ya Afrika Mashariki
Tunatoa rai kwa Kamati ya
bunge ya Mambo ya Nje na kamati ya ulinzi zichunguze suala hili linalohatarisha
mahusiano ya nchi zetu mbili kwa kuwa sio mara ya kwanza kwa mahusaiano haya
kutetereka
Nchi hizi mbili zina historia
iliyotukuka kimahusiano. Kwa upande wetu tuliunga mkono jitihada za Rais
Kikwete kulitangazia Bunge juu ya dhamira yake ya kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia na majirani zetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tunaendelea kutoa wito kwa
serikali kuchukua hatua za kidiplomasia na kuzingatia misingi y a sheria za
kimataifa ili kulinda hadhi ya taifa letu kimataifa na pia kusimamia misingi ya
sera zetu za mambo ya nje.
Imetolewa leo Februari 4, 2014 na;
Ezekia Wenje (MB)
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje-CHADEMA
No comments:
Post a Comment