Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian
Kaijage amesema kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe
la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia itakayochezwa keshokutwa (Ijumaa)
jijini Lusaka.
--------------
Akizungumza kwenye hafla ya kuiaga
timu hiyo iliyofanyika leo (Februari 12 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF jijini
Dar es Salaam, Kocha Kaijage amesema wachezaji wake wako vizuri, ingawa hakuwa
tayari kutoa ahadi kuhusu matokeo.
“Vijana wako vizuri, lakini sitaki kutoa
ahadi. Watanzania watuombee, watuunge mkono ili tuweze kufanya vizuri,” amesema
Kocha Kaijage katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi.
Twiga Stars inaondoka na kikosi cha wachezaji
19 na benchi la ufundi lenye watu watano kwa ndege ya Fastjet kwa ajili ya
mechi hiyo itakayooanza saa 9 kamili kwa saa za Zambia. Msafara wa timu hiyo
unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho
chini ya nahodha Sophia Mwasikili ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid,
Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa,
Fatuma Makusanya, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Happiness Mwaipata, Maimuna
Mkane, Mwapewa Mtumwa, Sherida Boniface, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena
Said.
Wakati huo huo, timu ya Azam imeondoka
leo alfajiri (Februari 12 mwaka huu) kwenda Beira, Msumbiji kwa ajili ya mechi
ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi Ferroviario da Beira itakayochezwa
Jumamosi. Msafara wa timu hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF, James Mhagama.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF, Nassib Ramadhan ataongoza msafara wa timu ya Yanga inayoondoka kesho
mchana kwenda Comoro kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
dhidi ya Komorozine itakayochezwa Jumamosi.
No comments:
Post a Comment