MWANAMKE
mkazi wa kijiji cha Ikandamoyo, wilayani Katavi, Veronica Saleh ‘Mama Kaela’
(50), amefanya uamuzi adimu wa kuolewa na wanaume wawili ambao anaishi nao
kijijini hapo.
Kijiji hicho kipo umbali wa takribani kilometa 30 kutoka mjini hapa katika Jimbo
la Katavi linalowakilishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Pamoja na ndoa hiyo iliyowezeshwa na mume mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo,
imeelezwa kuwa mwanamke huyo ndiye ‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa zaidi ya miaka
saba sasa, huku akiwa na amri kuu katika nyumba, kama ilivyo katika ndoa za
kawaida.
Wanaume hao ni Paulo Sabuni ‘Baba Kaela’ (60) ambaye ndiye mume mkubwa na
Arcado Mlele (45) ambaye ni mume mdogo.
Taarifa za kuwapo kwa ndoa hiyo ya aina yake, ziliifikia Globu ya Jamii na
kufanyiwa uchunguzi kwa zaidi ya wiki tatu, na hatimaye katikati ya wiki hii,
wahusika walikubali wao wenyewe kuzungumzia suala hilo. Kwa mujibu wa maelezo
ya mwanamke huyo ambaye alionekana kuwa msemaji wa familia hiyo, yeye na mumewe
mkubwa, walifika kijijini hapo miaka 24 iliyopita, wakitoka kijiji cha Usumbwa
mpakani mwa Chunya, Mbeya na Tabora.
Wakiwa kijijini hapo mume wake aliendelea kufanya kazi ya ukulima wakati yeye
mama (Veronica), pamoja na kilimo hujihusisha na upishi na uuzaji wa pombe ya
kienyeji iitwayo kayoga.
Mwanamke huyo ambaye amesema ana watoto wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka
16 (ambaye ameolewa) na wengine wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la sita
na mdogo ana miaka saba, amesema hana shida na waume wake.
Ingawa wanandoa hao walizungumza kwa hadhari, majirani walikiri kuwa mwanamke
huyo anaishi na wanaume hao wawili kwa amani na kwamba mwanamke huyo ndiye
mwenye sauti na si waume zake.
“Si siri tena sasa, tumeshawazoea, kwani wanaishi kwa amani ila yule mume mdogo
anaishi kwenye nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake, lakini anashinda kwa
mume mkubwa, ambapo inajulikana kijijini hapa kuwa ni nyumba kubwa. “Basi pale
ni mambo yote, kula na kunywa, mama huyu amewapangia zamu wanaume hao kama
afanyavyo mume mwenye wake wengi.
Ama kweli ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni,” alisema mkazi mmoja kwa
masharti ya jina lake kutoandikwa gazetini. Ilielezwa, kwamba wanaume hao wana
akili timamu na hawatumii kilevi cha pombe kama ilivyo kwa mke wao.
Hata hivyo, mume mkubwa anapewa sifa za upole tofauti na mume mdogo anayetajwa
kuwa mkorofi kiasi cha mara kadhaa kumchapa makofi mkewe anapomuudhi.
Majirani wanadai kwamba Mama Kaela na mumewe Paulo, walipofika kijijini hapo,
walipokewa na kuishi maisha ya kawaida, lakini baadaye mama huyo alianza kuwa
na uhusiano wa kimapenzi na Arcado, ambaye naye alilazimika kuachana na mkewe
wa ndoa anayefahamika kijijini hapo kwa jina la Mama Pere.
Ilielezwa na mashuhuda hao kwamba mume mkubwa alipobaini uhusiano huo, alikuja
juu, lakini mwanamke huyo inadaiwa alimweleza mumewe huyo, atake asitake lazima
wataishi wawili, vinginevyo ataachana naye, ndipo mume mkubwa alipokubali
kuishi na mume mwenza.
Katika maisha ya kawaida katika familia hiyo, inaelezwa kwamba katika baadhi ya
siku ikitokea kuwa mama huyo amechoka kupika, mume mdogo huchukua jukumu la
kupika na kumwandalia chakula na maji ya kuoga mume mkubwa.
“Lakini mara nyingi kwa mfano, ikiwa ni zamu ya mama huyo kulala kwa mumewe
mkubwa, basi humfulia nguo zake kisha anakwenda kwa mumewe mdogo nako anamfulia
nguo.
“Ndivyo wanavyoishi, nasi sasa tumewazoea ila yule mama ni mkali na ana sauti
pale kwake kwa wanaume wale ila tunaona kama ana wivu sana kwa huyu mdogo
ambaye naye pia ana wivu kwa mkewe huyo, labda anahofia kuwa mama huyo anaweza
kuongeza mwanamume mwingine,” anasema mmoja wa majirani hao.
Hakuna mazuri yasiyokuwa na machungu, japo familia hiyo inaelezwa kuwa na
amani, mtoto wao mdogo nusura avuruge uhusiano wa wanandoa hao, baada ya
kuibuka mzozo wakati wa maandalizi ya ubatizo wake.
Kwa sababu anazojua mama, ingawa inafahamika kuwa wote ni watoto wa mume
mkubwa, mke huyo katika hati za ubatizo aliandikisha ubini wa mtoto huyo kuwa
ni Mlele (akimaanisha kuwa mtoto wa mume mdogo), lakini mume mkubwa aliweka
pingamizi kanisani akidai yeye ndiye baba halali wa mtoto huyo.
Kwa mujibu wa mwanamke huyo, yeye na Arcado ni waumini wa madhehebu ya Katoliki
wakati Paulo ni Mpentekoste. Madai ya mzozo wa uhalali wa `ubaba’ wa mtoto
huyo, yalithibitishwa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, akiwamo mwalimu wa
dini wa Kigango cha Kanisa Katoliki Uruira, Mashaka Abel. Walisema miaka sita
iliyopita, mtoto huyo akiwa na umri wa mwaka mmoja, alifanyiwa taratibu za
ubatizo, lakini ilishindikana, kutokana na wanaume hao, kila mmoja kudai ndiye
baba mzazi wa mtoto.
“Lilikuwa jambo la kustaajabisha sana, kwani familia hiyo ilifanya maandalizi
yote ya sherehe ya ubatizo wa mtoto huyo, lakini siku hiyo kanisani wakati huo
ilikuwa ni kigango cha Katumba ambacho sasa ni Uruira, sakata lilianzia pale Padri
alipomwuliza mama wa mtoto huyo ubini wa mtoto naye akasema ni Mlele.
“Hapo ndipo mume mkubwa alipopinga na kudai kuwa mtoto yule si wa Arcado bali
wake na yeye ndiye baba halali. Padri hakuamini, aliuliza tena na tena na
majibu yakawa ni yale yale, ndipo ubatizo ukashindikana,” alisema Katekista
Abel.
Kazi ya kutafuta undani wa ndoa hiyo haikuwa rahisi kutokana na mazingira ya
woga na usiri uliokusudiwa kubaki, ambapo awali mama alisema kwamba mume wake
ni Paulo pekee japo siku ambayo mwandishi wa habari hizi alifika kijijini hapo
na baadaye nyumbani kwa wanandoa hao na kumkuta mume mdogo (Arcado akimsaidia
mkewe kukoroga pombe. Awali katika utambulisho, walidai kuwa ni mtu na mdogo
wake na kusita kuzungumzia maisha yao ya kifamilia.
Mke wao ambaye alionekana wazi kuwa ni msemaji mkuu alifoka na kuja juu, akidai
kuwa hayuko tayari kuzungumzia uhusiano wake na wanaume hao wawili, ingawa
alikiri kuwa wanaishi pamoja.
"Kwa hiyo umefunga safari yote hii kutoka huko ulikotoka ili uje kwangu
mie Veronica … nasema sitaki kabisa mtu kuja hapa na kutaka kunivurugia
mpangilio wa maisha yangu, kwanza nani alikueleza hayo, wambea wakubwa hao
yanawahusu nini watu hao?” alihoji.
“Mie mume wangu ni huyu Paulo basi … sasa leo umeniachia vurugu ndani ya nyumba
nitapigwa na huyo mume wangu Paulo, kwani mmenishikisha ugoni?” alifoka Mama
Kaela. Hata hivyo, mume mkubwa alidai kuwa hatamwadhibu mkewe huyo na kwamba
wataendelea kuishi pamoja na mdogo wake Arcado kwa amani. Hata hivyo, akina
mama wengi kijijini hapo wanalaani kitendo cha mama huyo kuishi na wanaume
wawili ambapo waliomba uongozi wa Kanisa uingilie kati, ili mama huyo aweze
kufunga ndoa na mume mmoja.
Lakini kwa upande mwingine, baadhi walimpongeza mwanamke huyo wakidai kuwa
kitendo hicho ni cha kijasiri kwa mwanamke, kumudu kuishi na wanaume wawili na
kuwa na mamlaka juu yao.
|
No comments:
Post a Comment