Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam linawataka wananchi wote waliojiandikisha kushiriki
kikamilifu kupiga kura ili kutekeleza haki yao ya msingi kikatiba ya kuwachagua
viongozi wanaowapenda. Hakuna sababu ya kuwa na hofu siku hiyo kwa vile Jeshi
la Polisi limejiandaa vya kutosha kuhakikisha kwamba kuna ulinzi, usalama na
utulivu katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na vituo
vyote vya kupigia kura.
Tumewasiliana na
uongozi wa juu wa Tume ya taifa ya Uchaguzi pamoja na Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi na kwa pamoja tumeweka mikakati ya kutosha ya kudhibiti aina yoyote ya
uvunjifu wa amani unaoweza kujikeza.
Kupitia taarifa za
kiintelijensia tayari tumebaini mbinu chafu zilizotaka kutekelezwa na watu
wachache za kutaka kuvuruga utaratibu mzuri uliowekwa na Tume ya Taifa uchaguzi.
Mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kuleta fujo au uvunjifu wa amani
wa aina yoyote watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Maagizo ya tume pamoja
na ya mkuu wa Jeshi la Polisi ya kuzuia mikusanyiko ya aina yoyote baada ya
siku ya mwisho ya kampeni tarehe 24/10/2015 yazingatiwe. Kwa ujumla hatutakuwa
na uvumilifu wa aina yoyote kwa mtu yeyote atakayejaribu kuwafanya watu waishi
kwa hofu kuanzia tarehe 25/10/2015 na badala yake sheria itachukua mkondo wake
na wanaohusika watakamatwa bila kufanya ajizi.
Makamanda wa Polisi wa
Mikoa ya Ilala, kinondoni na Temeke wamepewa maagizo ya kuhakikisha kwamba wananchi
katika maeneo yao wanalindwa kikamilifu ili kundi moja lisiwe tishio kwa kundi
lingine na wazingatie ushiriki katika uchaguzi wa makundi maalum ikiwa ni
pamoja na akina mama, walemavu na wazee
ambao wana haki sawa na makundi mengine kama vijana n.k. Kila kituo cha kupigia
kura kitakuwa na ulinzi wa kutosha wa Jeshi la Polisi ambapo pia taratibu zote
za kupiga kura na kuhesabu kura zitafanyika katika hali ya utulivu.
Kila mtu jijini Dar es
Salaam na Tanzania nzima ana wajibu wa kutunza amani na kutoa taarifa za mtu yeyote
au kundi lolote ambalo litaenda kinyume na katiba au sheria mbalimbali za nchi
ikiwa ni pamoja na sheria zinazolinda haki na demokrasia wakati wa uchaguzi mkuu.
Tunawaomba wananchi
wote washirikiane na Jeshi la Polisi bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa
ili kila anayestahili kupiga kura apate fursa sawa. Kushinda uchaguzi au
kushindwa iwe ni matokeo ya utekelezaji wa demokrasia hivyo tunawaomba watu wa
jiji la Dar es Salaam pamoja na watanzania kwa ujumla wawe wavumilivu na aidha
kupongezana au kupeana pole katika hali ya amani na utulivu kama ilivyozoeleka
katika chaguzi zilizopita.
Napenda kuwatoa
wasiwasi wapiga kura wote na watu wengine kwamba wasisite kutekeleza haki yao
kwani Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu katika hali ya weledi na uwezo wa
hali ya juu kukabiliana na tatizo lolote. Mikoa na Vikosi vyote vya Jeshi la
Polisi vimeandaliwa na kuwekwa tayari pamoja na kupata askari wa ziada,
vitendea kazi vya kutosha pamoja na matayarisho ya kila aina siku ya tarehe
25/10/2015 ikiwa ni pamoja na Helkopter za Polisi zitakuwa angani ili
kuwahakikishia wananchi usalama wao jijini Dar es Salaam.
NB:
Kutokana na maamuzi ya Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam chini ya jopo la Majaji watatu, baada ya maombi ya
Wakili wa vyama vya siasa vya upinzani mahakama hiyo imetoa hukumu na tafsiri
dhidi ya maombi ya wakili KIBATALA ambaye alitaka tafsiri ya watu kuzuiwa au
kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.
Katika hukumu hiyo ni kwamba hairuhusiwi
na ni marufuku kufanya mikutano eneo la upigaji kura ikiwa ni pamoja na kukaa
mita 200. Kutokana na hilo Jeshi la Polisi halitaruhusu mtu au kikundi chochote
kukaa au kukusanyika kwa kisingizio cha kulinda kura kwa kuwa mahakama ambayo
ni chombo cha kisheria imeshatoa tafsiri sahihi na kwamba kazi ya kulinda kura
ni ya mawakala wa vyama na si ya wapiga kura au wanachama wa vyama vya siasa. Yeyote atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment