Kikosi cha timu ya Taifa ya
Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium
Lager, kinatarajiwa kuwasili leo saa 8 usiku katika uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Mwl. JK Nyerere kikitokea nchini Chad kilipokuwa na mchezo
dhidi ya wenyeji jana jioni.
Msafara wa Taifa Stars unaongozwa
na mkuu wa msafara ambaye pia ni Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA),
Ravia Idarus Faina utaondoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa N’Djamena
saa 8 mchana kuelekea Addis Ababa nchini Ethiopia, kabla ya kuunganisha
ndege saa 4 usiku tayari kwa safari ya kurejea nyumbani Tanzania.
Stars inarejea nyumbani baada ya
kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya wenyeji Chad, bao lililofungwa na
nahodha Mbwana Samatta katika mchezo uliochezwa uwanja wa Omnisport
Idriss Mahaymat Ouya jijini N’Djamena katika mchezo wa kundi G kuwania
kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017.
Mara baada ya kuwasili jijini Dar
es salaam, kikosi cha Taifa Stars kitaingia moja kwa kwa moja kambini
katika hoteli ya Urban Rose iliyopo eneo la Kisutu kujiandaa na mchezo
wa marudano utakaochezwa siku ya Jumatatu ya Pasaka katika uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment