Ndugu
Wanahabari,
Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali ambalo si la kisiasa wala kibiashara
lenye kujibidiisha katika kutetea, kulinda na kuendeleza haki za binadamu na
utawala bora nchini. Kituo kimekuwa kikifuatilia mwenendo wa serikali na taasisi
zake ili kuhakikisha utendaji wa serikali unafuata misingi ya sheria na haki za
Binadamu kwa lengo la kuhakikisha kuwa utendaji wa serikali unakuwa na tija kwa
wananchi wake.
Ndugu
Wanahabari,
Tangu Serikali ya awamu ya tano
iingie madarakani, takribani mwaka mmoja sasa, kumekuwa na jitihada za lazima
za serikali yenyewe katika kupambana dhidi ya rushwa na ubadhirifu,nakuimarisha
uwajibikaji vitu ambavyo ni vichocheo muhimu katika ustawina maendeleo
ya nchi.Kwa upande mwingine kumekuwa na
ongezeko la uwazi katika utekelezaji wa baadhi ya shuguli za serikali jambo
ambalo kwa mapana yake ni zuri pia.
Hata hivyo jitihada hizo zimekuwa
na kasoro mbali mbali za kiutendaji , kiufundi na kisheria ambazo zimekuwa
zikitajwa mara kadhaa na wadau mbalimbali ikiwemo Kituo Cha Sheria na Haki za
Binadamu. Kikubwa zaidi katika haya yote ni ukiukwaji mkubwa wa Haki za
Binadamu katika matamko na,hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kuanzia
ngazi ya serikali za mitaa mpaka serikali kuu. Mambo haya ambayo kwa nadharia yanaonekana
ni mepesi ni hatari zaidi katika ustawi wa nchi ya kidemokrasia na sisi kama
watetezi wa haki za Binadamu hatutaacha kuyakemea vikali ili kujenga jamii
yenye haki na usawa.
vitendo hivyo ambavyo serikali
imeendelea kuvifumbia macho.
Ndugu
Wanahabari,
Ninyi mmekuwa mashahidi kwani ni
mara nyingi tumetoa matamko kukemea kauli zisizo afya kwa ustawi wa utawala wa
sheria na Haki za Binadamu, lakini viongozi wa serikali wameendelea kuziba
masikio na kuendelea kuvunja sheria na kukiuka haki za Binadamu, ili hali
wakiongoza kama miungu watu.
Sote tumeshuhudia kauli ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa katika ziara ya kuzungumza na
wananchi huko Kinondoni. Ndugu Makonda amemshambulia kwa maneno mtumishi wa
Manispaa ya Kinondoni, Bi. Rehema Mwinuka baada ya kumtolea matamshi ya kejeli
na kumnyima haki yake ya asili ya kusikilizwa na hata kujieleza. Makonda alinukuliwa
akimfokea Bi.Mwinuka “hawa ndio vichaa
tunaohangaika nao, toka hapa”.
Ndugu
wanahabari,
Tanzania ni nchi inayoheshimu
utawala wa sheria kwa mujibu wa Katiba ya waka 1977. Hivyo serikali yetu kwa
mujibu wa katiba hiyo ina mihimili mitatu
ambayo ni Serikali yenyewe, Bunge na mahakama . Katika utendaji chombo
kilichopewa mamlaka kusimamia haki na tafsiri ya sheria ni mahakama pekee.
Licha ya misingi hii ya kikatiba kuwepo viongozi wa serikali wamekuwa
wakichukua nafasi ya Mahakama na kuhukumu na kuwahesabu watuhumiwa kuwa na
hatia moja kwa moja pasipo kujua
wanakiuka misingi ya katiba waliyo apa kuilinda. Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania pamoja na mambo mengine inasema “ Mtu hata hesabiwa kuwa na hatia mpaka Itakapo thibitishwa na Mahakama
yenye mamlaka” Kitendo cha kuwahukumu watu mbele ya hadhara na kuwataja
majina kama wezi , wajinga, wasiokuwa na akili timamu na lugha zingine zisizo
na staha ni kudhalilisha utu wa mtu na kuvunja misingi ya Katiba.
Ndugu
wanahabari,
Tunasikitika kuwa mbali na Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kukemea kwa nguvu uvunjwaji huu wa sheria na
ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaofanywa na viongozi bado viongozi wetu
wameendelea kuwa wakaidi na kusahau kuwa dhamana waliyo nayo iko kwa mujibu wa
sheria na badala yake wanajiona miungu watu kama alivyojifafanua Mhe.
Makonda
kwa kusema “huna wa kukutetea mimi
nikisimama mahala Mungu amesimama”.Aina hii ya kauli haitarajiwi kutumika
kwa viongozi wa serikali ya Kidemokrasia . Kauli hizi ni aina ya kauli mbazo
zimekuwa zikitumika katika serikali zilizofuata mifumo ya kifashisti. Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 13(1) “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na
wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya
sheria.” Ibara hii ya katiba
inatushangaza kuona ni wapi viongozi wetu wanatoa mamlaka ya kujitangaza wao ni
Mungu na waliopo chini yao hawana haki ya utetezi.
Tunapenda
kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa katiba Ibara ya 8 (1) inatanabaisha kuwa;
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo -
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka
yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa
mujibu wa Katiba hii;”
Hivyo tunapenda kumkumbusha mkuu wa
mkoa Makonda kuwa yeye amepewa dhaman tu na wananchi na hivyo yeye si Mungu
kama anavyodhani.
Kanuni za utumishi wa Umma za mwaka
2014, Kanuni 107(1) na (2) zinaeleza bayana kama ifuatavyo: “107 (1)
Mtumishi wa umma anapofanya kosa kuhusiana na kazi yake, Katibu Mkuu au Mkuu wa
Taasisi au Mkuu wa Idara husika atapaswa kuzingatia kama kosa hilo ni la jinai
au ni la uvunjaji wa nidhamu za kazi au aina zote mbili.
(2)
Iwapo mtumishi atafanya kosa la kinidhamu, Katibu Mkuu au Mkuu wa Taasisi au
Mkuu wa Idara atampa taarifa ya dai hilo mtumishi husika na kupewa nafasi ya
kujieleza na baadae kuchukuliwa hatua muafaka. Taarifa ya mtumishi huyo
itawasilishwa kwa maandishi kwa Katibu wa chama cha wafanyakazi au mwakilishi
wa wafanyakazi aliyomo katika Kamati ya Uongozi.”
Kifungu hiki kinatanabaisha wazi kwamba
Mh. Makonda amekuwa akikiuka taratibu za
kisheria za uwajibishaji wa watumishi wa
serikali walio chini yake.
Hata
hivyo kauli hiyo ya matusi pia ni udhalilishaji mkubwa wa kijinsia ukizingatia
Dunia inaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na
watoto.
Ndugu Wanahabari,
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendelea kuwasihi viongozi wa serikali kutopuuza
misingi ya utawala wa sheria kwani kwa kufanya hivyo wanavunja haki za wengine
na kukiuka misingi ya utawala wa sharia na utawala bora.
Tunaamini
kwamba kuna watanzania wengi wanateseka
huko mitaani na wanahitaji msaada. Nia ya serikali kufanya ziara katika maeneo
mbalimbali inaweza kuwa ni njema sana katika kukuza uwajibikaji isipo kuwa tu
kama taratibu za kisheria na misingi ya utawala bora itazingatiwa katika zoezi
hilo. Ziara hizi zingetumika zaidi kugundua maeneo dhaifu na kupanga mikakati
ya kuboresha kuliko kugeuka kuwa mahaka za wazi ambazo zinaweza kuwa chombo
kikuu cha uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi
ya katiba yetu.
Hata
hivyo tunamtaka Ndugu Paul Makonda kumwomba radhi Bi. Rehema Mwinuka kwa
kumdhalilisha kwa matusi tena mbele ya hadhara. Tunaamini kwamba serikali
inaweza kutimiza azma zake bila kukiuka utawala wa sheria kwani kuongoza bila
kufuata katiba si ruhusa katika mfumo wa kidemokrasia.
Imetolewa na Dkt. Helen
Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji
Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu
No comments:
Post a Comment